1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kusimamia ulinzi wa Gaza licha ya mpango wa amani

Sylvia Mwehozi AFP, Reuters
27 Oktoba 2025

Israel imesisitiza jana kwamba itaendelea kusimamia usalama wa ndani ya Gaza licha ya kusaini makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani ya usitishaji vita ambayo yataruhusu upelekwaji wa kikosi cha kimataifa cha usalama.

Israel Jerusalem 2025 | Benjamin Netanyahu katika sherehe ya kuwakumbuka wanajeshi waliouawa
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Abir Sultan/AFP

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hapo jana kwamba Israel itaamua yenyewe wapi na lini watawashambulia maadui zake na ni nchi zipi zitaruhusiwa kutuma wanajeshi kulinda makubaliano ya kusitisha mapigano. Alikuwa akizungumza wakati wa kikao cha baraza lake la mawaziri jana Jumapili.

"Tunadhibiti usalama wetu wenyewe na tumeweka wazi kwamba kuhusu vikosi vya kimataifa, Israel itaamua ni vikosi gani havikubaliki kwetu  na hivyo ndivyo tunavyofanya na tutaendelea kufanya hivyo. Hili bila shaka linakubaliwa na Marekani pia, kama wawakilishi wake waandamizi walivyoweka wazi katika siku za hivi karibuni. Israel ni taifa huru, tutajilinda sisi wenyewe na tutaendelea kudhibiti hatima yetu".

Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani, huku vikosi vya Israel vikiondoka baada ya kumalizika kwa miaka miwili ya mapigano makali dhidi ya Hamas, kikosi cha kimataifa kinachotarajiwa kujumuisha nchi nyingi za Kiarabu au Kiislamu, kinatarajiwa kulinda usalama wa Gaza.

Makamu wa rais wa Marekani JD Vance na Waziri Mkuu Benjamin NetanyahuPicha: Nathan Howard/Pool/AFP/Getty Images

Hata hivyo, Israel inapinga jukumu lolote la mpinzani wake wa kikanda Uturuki huku Netanyahu chini ya upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wenye msimamo mkali katika serikali yake ya muungano wake ambao walikubali hata kusitisha mapigano, alichukua msimamo mkali hapo jana wakati mawaziri wa serikali walipokutana Jerusalem.

Israel imeondoa vikosi vyake ndani ya Gaza hadi kwenye kile kinachoitwa "Mstari wa Njano" kwa ajili ya makubaliano ya usitishaji vita lakini inasalia kudhibiti zaidi ya nusu ya eneo hilo, ikiidhinisha kila msafara wa misaada wa Umoja wa Mataifa unaopitia mipaka yake na imefanya angalau mashambulizi mawili tangu kusitisha mapigano.

Wakati huo huo picha za shirika la habari la AFP zilionyesha msafara wa Misri huko Gaza, ukipeleka waokoaji na mashine nzito kwa ajili ya kuharakisha utafutaji wa mabaki ya mateka wa Israel ambao Hamas inasema wamefukiwa chini ya vifusi vya eneo hilo la Wapalestina lililoharibiwa.

Malori ya mizigo midogo yakipeperusha bendera ya Misri yalisafirisha tingatinga na wachimbaji wa mitambo hadi Gaza, yaliambatana na malori yaliyokuwa yakielekea kwenye kamati ya misaada ya Misri yenye makao yake makuu Al-Zawayda. Msemaji wa serikali ya Israel Shosh Bedrosian alisema waziri Mkuu Netanyahu ameidhinisha kuwasili kwa timu hiyo kutoka Misri.

Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/IMAGO

Mashirika ya misaada yanalalamika kwamba misafara ya kibinadamu bado haina njia ya kutosha ya kufika Gaza ili kupunguza hali ya njaa katika sehemu za eneo hilo, na familia bado zimebanwa na njaa.

Hali za mateka

Kundi la Hamas limesisitiza kuwa lina nia ya dhati ya kurejesha miili 13 iliyobaki ya mateka ambapo limepanua zoezi la utafutaji wa miili hiyo jana jumapili katika maeneo mapya ya Ukanda wa gaza.

Miili hiyo inajumuisha Waisraeli 10 waliotekwa nyara wakati wa shambulio la Oktoba 7, 2023 lililosababisha vita, Mwisraeli mmoja aliyetoweka tangu 2014, Raia mmoja wa Thailand na mfanyakazi mmoja Mtanzania. Hamas tayari imewarejesha mateka 20 waliobaki walio hai na miili 15 ya mateka.

Lakini kundi hilo, limeonya kuwa linajitahidi kupata miili ya wengine katika magofu ya Gaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 68,500 wameuawa na mashambulizi ya Israel, kulingana na takwimu kutoka kwa wizara ya afya ya eneo linaloongozwa na Hamas. Hata hivyo, kulingana na msemaji wa Israel, Hamas wanafahamu wapi iliko miili ya mateka na kwamba wanahitaji kuongeza juhudi katika kuitafuta.