1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kuiadhibu Palestina kwa uanachama wa UNESCO

1 Novemba 2011

Baada ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuikubalia Palestina uanachama kamili, baraza la mawaziri la Israel linakutana hivi leo (01.11.2011) kuzungumzia la kufanya kujibu hatua hii.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riad al-Maliki (kushoto) na balozi wa Palestina kwenye UNESCO, Elias Sanbar.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riad al-Maliki (kushoto) na balozi wa Palestina kwenye UNESCO, Elias Sanbar.Picha: dapd

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa kile kinachoitwa "Jukwaa la Watu Wanane" linakutana jioni hii kujadiliana hatua za kuichukulia Palestina na UNESCO. Mkutano huo unawajumuisha mawaziri wanane muhimu kwenye Baraza la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

UNESCO imeikubalia Palestina uanachama kamili licha ya kuwepo kwa upinzani mkali kutoka Israel na Marekani. Marekani inachangia 22% ya bajeti ya Shirika hilo, na sasa mchango huo umekatwa moja kwa moja.

Sheria za Marekani zinaizuia nchi hiyo kuchangia taasisi yoyote ya kimataifa ambayo inaitambua Palestina kama taifa huru. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland, ameiita hatua hiyo ya UNESCO kama isiyokubalika.

"Kuikubalia Palestina kama mwanachama wa UNESCO, ni tendo la kujutia, la kitoto, na linachohujumu dhamira yetu ya pamoja ya kuwa na amani ya kweli na haki kwenye eneo la Mashariki ya Kati." Amesema Nuland.

Wajumbe wa UNESCO wakifurahia baada ya kuipitisha Palestina kuwa mwanachama kamili.Picha: dapd

Lakini wakati Marekani ikilaani hatua hii, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, Nabil Al-Arabi, amesema uamuzi wa Marekani kuikatia UNESCO michango ya kifedha, imemshitua sana.

"Hatua hii ya Marekani inatoa ishara mbaya ikiwa kweli inaweza kufanikisha mazungumzo ya amani." Amesema Al-Arabi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeipongeza Palestina kwa kukubaliwa uanachama wa UNESCO, na kuiita hatua hiyo kuwa ni "ishara ya uungwaji mkono wa kimataifa kwa haki za Wapalestina".

Marekani na Israel zilifanya kampeni kubwa dhidi ya uanachama wa Palestina kwenye UNESCO, huku Israel ikidai kuwa hicho kingelikuwa kitendo cha upande mmoja kujichukulia maamuzi peke yake. Lakini kufika jioni ya jana, mataifa 107 yalipiga kura ya kuikubalia Palestina kuwa mwanachama kamili wa Shirika hilo, huku 17 tu yakipinga na 52 yakijiepusha kupiga kura.

Akilihutubia Bunge mjini Tel Aviv hapo jana, Waziri Mkuu Netanyahu aliapa kuwa serikali yake haitakaa kimya katika wakati ambapo upande mmoja unachukuwa kile alichokiita "hatua za kuidhuru Israel".

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba mkutano wa leo wa Baraza la Mawaziri unazingatia hatua kadhaa za kuiadhibu Palestina. Likimnukuu afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Netanyahu, gazeti la Haaretz limesema hatua hizo zinajumuisha kuzidisha kasi ya ujenzi wa nyumba za walowezi na pia kuzuia uhaulishaji wa fedha za kodi kwa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Serikali ya Israel huenda pia ikaondoa ruhusa maalum ya kusafiri kirahisi ndani ya ardhi yake kwa wajumbe wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Waziri wa Fedha wa Israel, Yuval Steinitz, amekiambia kituo kimoja cha redio kuwa nchi yake inazingatia kuacha kabisa kushirikiana na Palestina na UNESCO yenyewe. Mchango wa Israel kwa UNESCO ni 2% tu ya bajeti ya shirika hilo.

Baada ya hapo jana kupata uanachama kamili wa UNESCO, sasa Palestina inaweza kuomba uanachama wa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, kama lile la Hatimiliki, la Afya, la Anga na au la Atomiki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW