1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kuichunguza kampuni yake ya ujasusi

21 Julai 2021

Israel imeunda timu ya mawaziri waandamizi itakayochunguza madai kwamba teknolojia ya ujasusi inayouzwa na kampuni inayohusika na masuala ya ujasusi wa kimtandao ya NSO kufuatia madai ya udukuzi.

Zypern | Pegasus Spyware | Webseite NSO Group
Picha: Mario Goldmann/AFP/Getty Images

Israel inaunda timu hiyo kuichunguza NSO ya nchini humo kwa madai kwamba imekuwa ikitumika kwa udukuzi wa kimataifa huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayedaiwa kulengwa na udukuzi wa hivi karibuni akitaka uchunguzi ufanyike. 

Timu hiyo ya mawaziri inangozwa na baraza la kitaifa la usalama, NSC, linaloripoti kwa waziri mkuu Naftali Bennett na linajumuisha wataalamu wengi, ikilinganishwa na wizara ya ulinzi, ambayo ndio msimamizi mkuu wa mauzo ya kampuni hiyo ya Israeli ya teknolojia ya ujasusi wa kimtandao ya NSO.

Mashirika makubwa ya habari ulimwenguni yameripoti wiki hii kuhusiana na udukuzi uliofanywa na kampuni hiyo kupitia programu yake ya Pegasus nchini Ufaransa, Mexico, India, Morocco na Iraq. Duru zenye uelewa wa juu kuhusu timu hiyo na ambazo zimeomba kutotambulishwa zimesema kuna uwezekano kwamba kampuni hiyo itawekewa vizuizi vipya katika mauzo ya programu hiyo.

Duru zimeongeza kuwa lengo hasa la timu hiyo ni kujaribu kujua kile kilichotokea, kuliangazia suala hilo zima na kujifunza.

Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Bennett, hajazungumzia chochote kuhusiana na udukuzi huo.Picha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Si NSO wala ofisi ya waziri mkuu Bennett waliokuwa tayari kuzungumzia chochote kuhusu suala hili, na hata katika hotuba ya waziri mkuu hii leo kwenye mkutano wa masuala ya udukuzi wa kimtandao, hakugusia chochote kuhusiana na kampuni hiyo ya NSO, na badala yake alizungumzia tu kitisho kinacholetwa na mashambulizi ya kimtandao.

Bennett alinukuliwa akisema "Kama waziri mkuu wa Israel, ninalitazama hili kama moja ya vitisho vya hali ya juu kabisa vya usalama wa taifa. Na ninadhani kwamba mashambulizi ya kimtandao kote ulimwenguni ni miongoni mwa vitisho vikuu vya ulimwengu wenyewe."

Sikiliza Zaidi:

19.07.2021 Matangazo ya Mchana

This browser does not support the audio element.

Katika hatua nyingine, rais wa Ufaransa aliyetajwa miongoni mwa wakuu wa mataifa 14 waliolengwa kwenye udukuzi huo ametoa mwito wa kufanyika  uchunguzi mpana kufuatia taarifa hizo, hii ikiwa ni kulingana na waziri mkuu Jean Castex alipozungumza na kituo cha televisheni cha nchini humo cha TF1 hii leo.

Kulingana na gazeti la Ufaransa la Le Monde namba ya simu ya Macron ilikuwa kwenye orodha ya watu waliolengwa kwenye udukuzi huo kwa niaba ya Morocco, ingawa Morocco yenyewe imekana madai hayo.

Ofisi ya rais Macron imesema iwapo taarifa hizo zitakuwa zina ukweli, watazishughulikia kwa umakini mkubwa.

Wasiwasi umezidi kuongezeka kufuatia kitisho hicho, wakati Umoja wa Mataifa nao ukisema unafanya majadiliano na serikali ya Marekani kuhusiana na suala hilo. Umoja huo umesema kila udukuzi uliofanywa katika mawasiliano ya wakuu hao ni suala nyeti na linalotia wasiwasi mkubwa.

Soma Zaidi Kampuni ya teknolojia ya ujasusi ya Israel yadaiwa kuwadukua miongoni mwa wengine waandishi habari duniani

Mashirika: RTRE/DPAE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW