1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel kushinikiza usitishwaji vita Gaza kupitia Qatar

Hawa Bihoga
26 Februari 2024

Ujumbe wa Israel leo umeelekea Qatar kwa ajili ya mazungumzo ya kushinikiza makubaliano ya kusitisha vita katika eneo la Ukanda wa Gaza, ambalo vikosi vyake vimekuwa vikiendesha mashambulizi makali ya kijeshi.

Tel Aviv, Israel | Maandamano ya kushinikiza kuachiwa kwa mateka wa Israel
Maandamano ya kutaka kuachiliwa kwa mateka wa israel wanaoshikiliwa na Hamas Ukanda wa GazaPicha: Ohad Zwigenberg/picture alliance/AP

Israel inayokabiliwa na shinikizo kutoka kwa mshirika wake mkuu Marekani leo imewapeleka maafisa wake nchini Qatar, kushughulikia hatua zitakazowezesha kusimaisha vita katika ukanda wa Gaza na pia juu ya mpango wa kuachiliwa mateka, ambao Marekani inasema uko karibu kufikiwa. Marekani inaitaka Israel kufikia makubaliano ili kuepusha operesheni kubwa ya kijeshi katika mji wa Rafah. 

Chanzo kutoka serikali ya Israel kimesema ujumbe wa Israel unaoundwa na maafisa kutoka jeshi la shirika la ujasusi la Mossad, umepewa jukumu la kuunda kituo cha operesheni za kusaidia majadiliano.

Majukumu yake yatakuwa pamoja na kuchuja orodha ya wapiganaji ambao kundi la Hamas linawataka waachiliwe kama sehemu ya mkuabaliano ya kuwaachia mateka.

Ujumbe huo wa Israel unaashiria kwamba mazungumzo ya amani katika vita vya Gaza yako karibu zaidi kuliko wakati wowote tangu shinikizo kubwa mwanzoni mwa mwezi Februari, wakati Israel ilipokataa pendekezo la Hamas la kipindi cha miezi minne na nusu cha usitishaji vita.

Soma pia:Wapatanishi wa Israel waelekea Qatar

Wiki iliyopita, maafisawa Israel walijadili masharti ya kuwaachiliwa mateka wakati wa mazungumzo mjini Paris na ujumbe kutoka Marekani, Misri na Qatar, bila kuihusisha Hamas.

Duru za kiusalama za Misri zimesema mazungumzo ya kujongeleana yanayohusisha ujumbe kutoka Israel na Hamas - ambao utakutana kupitia wapatanishi katika mji sawa lakini siyo ana kwa ana - yatafanyika wiki hii, yakianzia nchini Qatar, na baade mjini Cairo.

Israel haijatoa tamko rasmi kuhusu mazungumzo hayo na hakukuwa na kauli ya mara moja kutoka kwa wenyeji Qatar siku ya Jumatatu.

Pande mbili zinasigana kufikia makubaliano

Hadharani pande hizo zinasalia na tofauti kubwa kuhusu malengo yao makuu: Hamas, ambayo inatawala Ukanda wa Gaza, inasema haitawaachilia zaidi ya mateka 100 ambao bado inawashikilia hadi Israeli iahidi kujiondoa kikamilifu Gaza na kumaliza vita.

Israel nayo inasema itajadiliana tu usitishaji wa muda wa vita kwa ajili ya kuwachiwa mateka wake, haitasitisha kikamilifu kampeni yake ya ardhini hadi Hamas itakapotokomezwa, na inataka udhibiti wa usalama wa Gaza kwa muda usiojulikana.

Aliekuwa Waziri Mkuu wa mamalaka ya Plestiana Mohammad ShtayyehPicha: Ayman Nobani/dpa/picture alliance

Katika hatua ambayo inaweza kuwa na athari katika mazungumzo ya muda mrefu ya kumaliza mzozo huo, waziri mkuu wa Mamlaka ya Palestina, ambayo ina udhibiti mdogo wa kiraia katika sehemu za Ukingo wa Magharibi, amejiuzulu leo Jumatatu.

Soma pia:Waziri mkuu wa Palestina ajiuzulu

Mohammad Shtayyeh amesema anajiuzulu ili kuruhusu maelewano mapana kati ya Wapalestina kuhusu mipango ya kisiasa kufuatia vita vya Gaza.

"Naona kwamba hatua inayofuata na changamoto zake zinahitaji mipango mipya ya kiserikali na kisiasa ambayo inazingatia ukweli unaojitokeza katika Ukanda wa Gaza," alisema katika sehemu ya hotuba yake

Aliongeza kwa "mazungumzo ya umoja wa kitaifa, na uhitaji wa dharura wa maafikiano baina ya Wapalestina kwa msingi wa kitaifa, ushiriki mpana, umoja na upanuzi wa mamlaka ya Mamlaka ya Palestina juu ya ardhi yote ya Palestina."

Mamlaka ya Palestina, inayotambuliwa na nchi za Magharibi kama mwakilishi rasmi wa Wapalestina, ilipoteza udhibiti wa Gaza kwa Hamas mwaka 2007.

Washington imetoa wito wa mageuzi ndani ya mamlaka hiyo kama sehemu ya ufumbuzi jumla wa usimamiziwa maeneo yote ya Palestina ukiwemo Ukanda wa Gaza baada ya vita.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW