1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yaiambia ICJ 'Israel laazima izuwiwe'

16 Mei 2024

Afrika Kusini imeiomba mahakama ya juu ya UN kuamuru usitishaji wa operesheni ya Rafah kama sehemu ya kesi yake inamoituhumu Israel kwa mauaji ya halaiki, ikisema nchi hiyo laazima izuwiwe.

Uholanzi | Mahakama ya Kimataifa kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati
Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola na Balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi Vusimuzi Madonsela katika mahakama ya ICJ katika moja ya kesi za mauaji ya halaiki dhidi ya Israel.Picha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP/Getty Images

Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa, ICJ, imeanza kusikiliza shauri lililowasilishwa na Afrika Kusini ikiitaka kuishinikiza Israel kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza, ambako zaidi ya nusu ya wapalestina wametafuta hifadhi.

Afrika Kusini imeiambia mahakama hiyo katika siku ya kwanza ya kusikiliza shauri hilo siku ya Alhamisi, kuwa mauaji ya kimbari yanaendelea Gaza, wakati ambapo Israel ikisema wanajeshi zaidi wataingia Rafah.

Hii ni mara ya nne kwa Afrika Kusini kuiomba mahakama ya haki ya kimataifa kuidhinisha hatua za dharura tangu taifa hilo lilipoanzisha mashauri dhidi ya mashambulizi likidai kuwa hatua za kijeshi za Israel katika vita vyake na wanamgambo wa Hamas Gaza vimegeuka mauaji ya halaiki.

Soma pia: Marekani yaihimiza korti ya UN kutoiamuru Israel kukomesha ukaliaji wa ardhi za Wapalestina

Kulingana na ombi la karibuni zaidi, maagizo ya muda yaliotolewa awali na mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, yalikuwa hayatoshi kushughulikia mashambulizi ya kikatili dhidi ya Rafah, ambayo ndiyo hifadhi iliyosalia kwa watu wa Gaza.

Israel inaitaja Rafah kuwa ngome ya mwisho ya Hamas, ikipuuza maonyo kutoka Marekani na washirika wake wengine kwamba operesheni yoyote kubwa dhidi ya mji huo itasababisha janga kubwa kwa raia.

Wawakilishi wa kisheria wa serikali ya Israel wakiwa katika mahakama ya Umoja wa Mataifa, ICJ kutoka utetezi wao dhidi ya tuhuma za mauaji ya halaiki kufuatia vita vya Gaza.Picha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP/Getty Images

Maombi ya Afrika Kusini kwa ICJ

Afrika Kusini imeiomba ICJ kuiamuru Israel kuondoa wanajeshi wake Rafah na kuhakikisha maafisa wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya misaada na waandishi habari wanaingia Gaza pasina vikwazo vyovyote, na kuripoti juu ya utekelezaji wa maagizo hayo ndani ya wiki moja.

Katika shauri lililoswasilishwa mapema mwaka huu, Israel ilikanusha vikali tuhuma za kufanya mauaji ya halaiki Gaza na kusema inafanya kila iwezalo kuepusha vifo vya raia na kwamba inalenga tu wapiganaji wa Hamas. Inadai mbinu ya Hamas ya kujificha miongoni mwa raia inafanya iwe vigumu kuepusha vifo vya raia.

Mnamo mwezi Januari, majaji wa ICJ waliiamuru Israel kufanya kila iwezavyo kuzuwia vifo, uharibifu na vitendo vya mauaji ya halaiki Gaza, lakini jopo la majaji hao lilishindwa kuamuru kukomeshwa kwa operesheni hiyo ya kijeshi ambayo imeangamiza sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza.

Katika amri ya pili mwezi Machi, mahakama hiyo ilisema Israel inapaswa kuchukuwa hatua za kuboresha hali ya kibinadamu Gaza, ikiwemo kufungua vivuko zaidi vya ardhini kuruhusu ugavi wa chakula, maji, mafuta na mahitaji mengine.

Vifaru vya Israel vikiwa vimekusanyika karibu na mpaka wake na Gaza.Picha: Abis Sultan/EPA

Israel yakaidi miito ya washirka

Hata hivyo waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema katika matamshi yaliotolewa na ofisi yake hii leo, kwamba wanajeshi zaidi wataingia Rafah kuendeleza operesheni hiyo, ambayo shirika la wakimbizi wa Kipaletina UNRWA, limesema tayari imesababisha watu 600,000 kuikimbia Rafah.

Soma pia: Waziri wa Wapalestina aishutumu Israel kwa ubaguzi wa rangi

"Operesheni hii itaendelea. Hamas siyo shirika linaloweza kujipanga tena kwa wakati huu, haina wanajeshi wa akiba, haina uwezo wa kuzalisha risasi, haina ugavi, haiwezi kupata silaha mpya, haiwezi kuwatibu magaidi tuliowapiga. Matokeo ni kwamba tunaidhoofisha,"alisema Gallant.

Na katika upande wa kaskazini wa Gaza, vifaru vya Israel vimeendela kukabiliana na mashambulizi ya maroketi ya wapigaji wa Hamas na wahsirika wao wa Islamic Jihad waliojichimbia huko.

Matawi ya kijeshi ya makundi hayo yamefanikiwa kupambana kaskazini na kusini mwa Gaza, yakitumia mahandaki yenye ulinzi mkali kufanya mashambulizi kote kaskazini, ambayo ndiyo ilikuwa kiini cha uvamizi wa kwanza wa Israel, na nyanja mpya za mapigano kama Rafah.

Kwanini Afrika Kusini inaishtaki Israel ICJ?

02:26

This browser does not support the video element.

Bahrain yaitisha mkutano wa amani wa Mashariki ya Kati

Akizungumza katika siku ya kwanza ya Mkutano wa Kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu uliogubikwa na vita vya Israel na Hamas hii leo, Mfalme wa Bahrain,  Hamad bin Isa Al Khalifa, ametoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa amani wa kanda ya Mashariki ya Kati, mbali ya kutambua kikamilifu uwepo wa taifa la Palestina na kukubaliwa uanachama wake ndani ya Umoja wa Mataifa.

Soma pia: Kesi ya mauaji ya halaiki ya Afrika Kusini dhidi ya Israel inahusu nini?

Maafisa wa afya wa Gaza wanasema idadi ya vifo kutokana na vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miezi saba saba sasa imefikia 35,272, na hali ya utapiamlo imeendea wakati ambapo juhudi za msaada wa kimataifa zimekwamishwa na vurugu, pamoja na hatua ya Israel kufunga kivuko chake cha Kerem Shalom, pamoja na kivuko cha mpakani cha Rafah, kati ya Gaza na Misri.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW