Israel: Mahakama kuanza kusikiliza kesi mabadiliko ya sheria
12 Septemba 2023Mnamo Julai 24, mwaka huu wa 2023, serikali ya mseto ya mrengo mkali wa kulia nchini Israel ilipitisha marekebisho ya katiba kwa kura 64 bila ya upinzani kwenye bunge la Israeli.
Hapakuwapo kura za kupinga marekebisho hayo kwa sababu wapinzani walitoka nje ya bunge kuashiria kutokubaliana nayo.
Hiyo ilikuwa duru ya kwanza katika mabadiliko ya sheria ya msingi.
Baada ya kura hiyo, mashirika kadhaa ya kiraia, mabaraza ya raia, vyama vya upinzani na wananchi binafsi waliwasilisha malalamiko kwenye mahakama kuu ya haki kupinga marekebisho hayo na ikiwezekana yabatilishwe.
Soma pia:Israel yapeleka polisi wengi eneo la maandamano
Mahakama ya juu nchini Israel itayasikiliza malalamiko hayo leo Jumanne.
Jambo maalum kuhusu kusikilizwa kwa shauri hilo ni kwamba kwa mara ya kwanza majaji wote 15 watahudhuria.
Vyombo vya habari nchini Israel vimesema hatua hiyo haina kifani. Kwa kawaida ni kati ya majaji watatu na tisa wanaoshiriki.
Kuhudhuria kwa majaji wote 15 kunathibitisha umuhimu mkubwa wa shauri hilo.
Msingi wa maamuzi utazingatia nini?
Mahakama italazimika kuamua iwapo itapunguza mamlaka yake. Hadi sasa, mahakama imejizuia kupinga sheria ya msingi, ambayo hutumika kama katiba.
Ingawa tangazo la uhuru wa Israel mwaka 1948 lilitoa wito wa kupitishwa katiba, nchi hiyo mpaka sasa haina katiba.
Badala yake, sheria ya msingi ya kwanza ilipitishwa bungeni mnamo mwaka 1958 baada ya kufikiwa mwafaka.
Hadi sasa, sheria 13 za msingi zinatumika kama marejeleo ya katiba. Sheria hizo 13 zinafafanua wazi vipengele vya msingi vya mfumo wa kidemokrasia na utawala na haki za kiraia nchini Israel.
Soma pia:Bunge la Israel lapitisha sheria tata ya mageuzi ya mahakama
Mchakato wote wa kuyasikiliza malalamiko ya wapinzani utatangazwa moja kwa moja.
Marekebisho ya sheria ya msingi katika mahakama yanabatilisha kile kinachoitwa kiwango cha busara.
Inaondoa uwezo wa mahakama ya juu ya Israeli na mahakama nyingine kufanya mashauri na kutoa hukumu dhidi ya maamuzi ya serikali na wizara zake.
Kulingana na marekebisho yaliyofanywa na serikali, sheria inayokusudiwa itatumika katika uteuzi wa nyadhifa za kisiasa, au inapohusu kuachishwa kazi katika nyadhifa za juu.
Kipi kitapunguza mamalaka ya mahakama?
Wapinzani wa mabadiliko hayo wanahoji kwamba yatapunguza mamlaka ya mahakama kuweza kuyachunguza maamuzi ya maafisa wa serikali.
Kwa mfano, itakuwa vigumu kwa mahakama ya juu kuwalinda watumishi waandamizi wa serikali katika kesi za kuwafuta kazi kiholela, au kuwafuta kazi kwa sababu za kisiasa.
Wanaoyaunga mkono mabadiliko ya sheria hiyo ya msingi wanadai kwamba yatazuia pande fulani kujiingiza katika maamuzi yanayotolewa na maafisa walioteuliwa.
Wanasema kujiingiza huko kunahujumu msingi wa kidemokrasia wa utawala wa wengi.
Soma pia:Hotuba ya Netanyahu yaibua maandamano mapya Israel
Kwa upande wao, wapinzani wa marekebisho wanahoji kwamba mabadiliko hayo yanahujumu msingi wa demokrasia nchini Israel. Pia wanasema yataathiri mgawanyo wa mamlaka na kufanya iwe vigumu kuidhibiti serikali.
Hakuna anayetarajia uamuzi wa haraka juu ya malamiko ya wapinzani wa marekebisho.
Wengi wanatarajia uamuzi kutolewa baada ya siku kuu za kiyahudi kuanzia kati kati ya mwezi huu au kabla ya kujiuzulu kwa rais wa mahakama kati kati ya mwezi wa Oktoba.
Uamuzi huo utategemea na idadi ya majaji watakayaounga mkono au kuyapinga marekebisho yaliyofanywa na serikali ya mseto ya mrengo mkali wa kulia.
Nchini Israel imeionya Mahakama ya Juu isiingilie kati mfumo wa marekebisho ya mahakama wenye utata, kabla ya mahakama ya juu kutoa uamuzi wake.