1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Miaka 63 ya kwenda ukimbizi Wapalastina

Miraji Othman13 Mei 2011

Israel yaadhimisha miaka 63 tangu kuundwa na Wapalastina walikumbuka janga hilo.

Kambi ya wakimbizi wa Kipalastina katika Ukanda wa GazaPicha: Maik Meuser

Majeshi ya Israel leo yako katika hali yqa tahadhari kubwa kukihofiwa kutatokea michafuko wakati Wapalastina wanalikumbuka janga lilowafika mwaka 1948 pale ilipoundwa dola ya Israel. Zaidi ya Wapalastina 760,000 leo pamoja na vizazi vyao wanakisiwa kufikia milioni 4.7 walifukuzwa kutoka makwao na kulazimika kwenda uhamishoni kutokana na mzozo uliofuata kuundwa dola ya Israel. Zaidi anayo Othman Miraji.

Msemaji wa polisi huko Israel amesema polisi wako katika hali ya tahadhari kubwa, na maelfu ya polisi wamewekwa ndani na kuuzunguka mji wa Jerusalem, pamoja na sehemu za kaskazini. Msemaji huyo alisema kwa sasa hawatazamii kutatokea chochote, lakini wanataka kuhakikisha kwamba hakutakuweko fujo katika eneo la Msikiti wa al-Aqsa. Eneo hilo sio tu ni takatifu kwa Waislamu, umuhimu wake ukifuata  Misikiti ya Makkah na Madinah, lakini pia ni mahala patakatifu kwa Wayahudi. Maelfu ya Waislamu wanatarajiwa kufika leo katika Msikiti wa al-Aqsa kwa sala ya ijumaa. Lakini polisi walisema kwamba kwa vile leo pia inakumbukwa siku ya al-Naqba-, kuhama kwa wingi Wapalastina baada ya kuundwa dola ya Israel, polisi wataweka vizuizi na watawaruhusu tu wanaume walio na zaidi ya umri wa miaka 45 na walio na vitambulisho vya buluu vya Israel kuingia katika eneo hilo. Wanawake hawatazuiliwa.

Makaazi ya Wapalastina katika kambi yao mjini Tripoli, LebanonPicha: picture-alliance/dpa

Wapalastina pamoja na Waarabu wanaoishi Israel leo wanatarajiwa kuanza kufanya milolongo ya maandamano kuikumbuka kwa huzuni siku ya al-Nakba. Kilele cha makumbusho hayo kitafikiwa jumapili ijayo.

Wanaharakati nyuma ya ule mtandao wa Internet ulio na jina la Intifada ya Tatu wamewahimiza Wapalastina wajiunge na uasi mpya, waandamane na kwenda katika majumba ambayo waliyakimbia au kulazimishwa kuyahama pale Israel ilipoundwa mwaka 1948

Wakimbizi wa Kipalastina walioko Misri, Lebanon, Jordan na Syria pia wataikumbuka siku hiyo kuanzia leo.

Polisi ya Israel imesisitiza kwamba wao watachukuwa hatua kali kuzuwia jaribio lolote la kutaka kuchafua usalama wa umma kutoka kwa mtu yeyote.

 Jumanne iliopita, Israel ilisheherekea mwaka wa 63 tangu kuundwa, kwa mujibu wa kalenda ya kiyahudi.

Licha ya  zaidi ya Wapaalstina 760,000- kwa makisio ya sasa pamoja na vizazi wao wanaotimia milioni 4.7- waliondoka Palastina wakati huo, lakini 160,000 walibakia na kuja kujulikana kuwa ni Waarabu wa Israel. Hivi sasa pamoja na vizazi vyao wanakisiwa kutimia watu milioni 1.3, hivyo kufanya asilimia 20 ya wakaazi jumla wa Israel.

Maisha Israel imekataa kurejea wakimbizi wa Kipalastina waliofukuzwa mwaka 1948, ikihofia kwamba kurejea kwa wingi watu hao katika maeneo yao ya asili kutahatarisha wingi wa Wayahudi katika Israel, ambako sasa kuna Wayahudi milioni 5.8. Na kwa mujibu wa  ofisi kuu ya takwimu ya Palastina ni kwamba kuna Wapalastina milioni 11 duniani kote, milioni 5.5 wanaishi sasa katika Ukingo wa Magharibi na katika Ukanda wa Gaza. Wakati inatarajiwa mwaka 2014 Warabu wa Kipalastina na wayahudi wa Israel watakuwa sawa kwa sawa kwa idadi, kila upande ukiwa na watu milioni 6.1, lakini itakapofika mwaka 2020 Wapalastina wanatarajiwa kufikia idadi ya milioni 7.2 na Wayahudi kuwa milioni 6.7.

Msikiti wa al-Aqsa na maeneo ya ibada ya Wayahudi mjini JerusalemPicha: dpa

Wakimbizi wengi wa Kipalastina, zaidi ya asilimia 60, wanaishi Jordan, Syria na Lebanon. Zaidi ya asilimia 16 wanaishi katika Ukingo wa Magharibi na asilimia 23 katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi: Miraji Othman/AFP/dpa

Mhariri: Yusuf, Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW