1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel na Hamas waendelea kubadilishana mateka na wafungwa

29 Novemba 2023

Israel na kundi la Hamas zimeitumia siku ya kwanza kati ya siku mbili za kurefushwa mkataba wa kusitisha mapigano kuendelea kubadilishana mateka na wafungwa.

Israel | Ubadilishanaji mateka kati ya Israel na Hamas
Tangu kuanza usitishaji mapigano, zaidi ya mateka 80, wengi wakiwa raia wa Israel wameachiwa na kundi la Hamas.Picha: Israel Defense Forces/REUTERS

Hayo yameshuhudiwa wakati hali ya mashaka inaongezeka juu ya nini kitatokea baada ya muda huo wa siku mbili kumalizika leo Jumatano.

Katika siku ya kwanza jana Jumanne, mateka 10 wa Kiisraeli waliachiwa huru na kundi la Hamas. Idadi hiyo inajumuisha wanawake 9 na msichana wa miaka 17.

Kundi la Hamas limewaachia huru pia raia wawili wa Thailand. Kundi hilo la mateka 11 lilikabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu kabla ya kupokelewa na mamlaka za Israel.

Muda mfupi baadae, Israel nayo iliwaachia huru wafungwa 30 wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa kwenye moja ya jela zake.

Mateka 81, wafungwa 180 waachiwa chini ya mkataba wa kusitisha mapigano 

Tangu kuanza usitishaji mapigano Israel imewaachia huru Wapalestina 180 waliokuwa wakishikiliwa kwenye jela za nchi hiyo.Picha: Muammar Awad/Xinhua/picture alliance

Tangu kuanza usitishaji mapigano Ijumaa iliyopita kundi la Hamas kwa jumla limewaachia huru mateka 81, wengi wakiwa raia wa Israel. Kwa upande mwingine Israel nayo imewaachia wafungwa 180 wa Kipalestina.

Muda huo wa kusitisha mapigano umewezesha pia kuingizwa msaada mkubwa wa kiutu kwenye Ukanda wa Gaza eneo linalokabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na mashambulizi ya Israel yaliyoingia wiki ya saba.

Israel ilianzisha hujuma hizo mnamo Oktoba 7, saa chache baada ya kundi la Hamas kufanya shambulizi kubwa lililowauwa watu 1,200 ndani ya ardhi ya Israel.

Tangu wakati huo, takwimu za mamlaka za Ukanda wa Gaza zinasema zaidi ya watu 14,000 wameuwawa kutokana na mashambulizi makali ya ardhi na angani yanayofanywa na vikosi vya Israel.

Israel imesema dhamira ya operesheni hiyo ni kulitokomeza kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza na ambalo nchi hiyo pamoja na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kadhaa ya magharibi yameliorodhesha kuwa la kigaidi.

Mashaka yatawala siku ya mwisho ya  muda wa kusitisha mapigano

Wakati siku mbili zaidi za kusitisha vita zinaelekea kumalizika leo, mashaka ni makubwa juu ya kuanza tena hujuma nzito za Israel kwenye Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Jacquelyn Martin/Pool via REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekwishasema kampeni yake ya kijeshi itaendelea baada ya muda wa sasa wa usitishaji mapigano kumalizika.

Akizungumza na kituo cha utangazaji cha Ujerumani, Welt Tv, Netanyahu amesema Israel haina chaguo jingine isipokuwa kupambana dhidi ya Hamas na kulitokomeza kundi hilo.

Licha ya matamshi hayo ya Netanyahu, juhudi bado zinafanyika kufanikisha makubaliano mengine ya kurefusha muda wa kusitisha mapigano lakini hakuna juhudi zozote alau kwa hivi sasa za kukomesha kabisa operesheni ya Israel huko Gaza.

Duru zinasema majadiliano yanaendelea nchini Qatar yakiwahusisha viongozi wa mashirika ya ujasusi ya Israel, Marekani na maafisa wa Misri kujaribu kufikia makubaliano mapya ya kusitisha mapigano.

Misaada zaidi yatumwa Ukanda wa Gaza kupunguza madhila 

Misaada karibu yote inaingia Gaza kupitia mpaka na Misri wa RafahPicha: Saudi Press Agency/dpa/picture alliance

Wakati huo huo misaada zaidi imendelea kupelekwa Ukanda wa Gaza kuwasaidia raia wanaopitia hali ngumu ya kukosa mahitaji muhimu ikiwemo chakula.

Marekani imesema imesafirisha kwa ndege zaidi ya kilo 50,000 za chakula na vifaa vya matibabu kwenda Gaza. Shehena hiyo ni ya kwanza kati ya awamu tatu za misaada inayotarajiwa kupelekwa Gaza kutoka Washington.

Uturuki nayo imesema inatumai itakamilisha hivi karibuni ujenzi wa hospitali za muda ndani ya Ukanda wa Gaza na kuanza kutoa huduma mara moja.

Hayo yametangazwa na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Fahrettic Koca baada ya ujumbe wa Uturuki kuingia Gaza kupitia mpaka wa Rafah kwa ajili ya kutathmini maeneo yanayofaa kujengwa hospitali hizo.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW