1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Hamas wafikia makubaliano ya kubadilishana mateka

22 Novemba 2023

Viongozi wa dunia wapongeza makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Israel na Hamas. Makubaliano hayo yatasababisha kuachiliwa kwa baadhi ya mateka wa Israel huku mapigano yakisimamishwa kwa muda wa siku nne.

Israel | Mwanamke akiangalia picha za mateka wa Israel
Israel | Mwanamke akiangalia picha za mateka wa IsraelPicha: Oded Balilty/AP/picture alliance

Kulingana na Israel, mateka 50 wa nchi hiyo waliotekwa na kundi la wanamgambo wa Hamas wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 wataachiliwa.

Mateka wote watakaoachiliwa ni wanawake na watoto. Kwa upande wa Hamas, wamesema Israel itawaachilia wanawake na watoto wa Kipalestina 150 wanaoshikiliwa katika jela za Israel.

Makubaliano hayo pia yanajumuishakusitisha mapigano kwa siku nne. Israel imesema itaongeza muda wa kusitisha mapigano kwaziada ya siku moja kwa kila mateka 10 watakaoachiliwa na Hamas.

Soma:Viongozi wa dunia wapongeza makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Istrael na kundi la Hamas

Hata hivyo kabla ya kuidhinishwa kwa makubaliano hayo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alisisitiza kwamba kusitisha mapigano hakutamaanisha mwisho wa vita dhidi ya kundi la Hamas.

Rais wa Marekani Joe Biden amesemaameyapokea vyema makubaliano ambayo yatafanikisha kuachiliwa kwa mateka waliochukuliwa na Hamas wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel, na ameongeza kuwa mateka wa Marekani watakuwa miongoni mwa watakaoachiliwa.

Rais huyo wa Marekani amezishukuru Misri na Qatar kwa kusaidia katika upatanishi kati ya Israel na kundi la Hamas.

Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani amesema anatumai mpango huo wa kubadilishana watu waliotekwa nyara utawezesha kufikiwa mchakato wa amani katika Ukanda wa Gaza.

Mahmud: Wapalestina wanathamini juhudi za upatanishi

Rais Mahmud Abbas na uongozi wa mamlaka ya Palestina wamesema wamependezwa na makubaliano yaliyofikiwa na amesema wapalestina wanathamini juhudi za usuluhishi zilizofanywa na Qatar na Misri.

Mahmoud Abbas ametoa wito wa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu mzozo kati ya Israel na Palestina.

Soma:Baraza la mawaziri la Israel laidhinisha makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka

Naye waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameungana na viongozi wa dunia katika kukaribisha hatua ya kufikiwa makubaliano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas. Amesema hayo ni mafanikio makubwa na amehimiza juu ya kutumia kipindi chakusimamishwa mapigano kupeleka msaada muhimu kwa watu wa Gaza.

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema ameiamuru Tume yake ya Ulaya kuongeza upelekaji wa misaada huko Gaza kufuatia tangazo la kusitishwa mapigano kwa siku nne.

Mzozo wa Mashariki ya Kati wakaribia mwezi mmoja

01:17

This browser does not support the video element.