1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel na Hamas zaendelea kushambuliana huko Gaza

Sylvia Mwehozi
17 Oktoba 2023

Israel imeyashambulia maeneo ya kusini mwa Ukanda wa Gaza huku wanamgambo wa Hamas nao wakiendelea kufyatua maroketi kuelekea miji kadhaa ya Israel.

Ukanda wa Gaza
Watu wa Gaza wakipita katika eneo lililoharibiwa na mashambulizi ya IsraeliPicha: Middle East Images/ABACA/IMAGO

Tukianzia Gaza kwenyewe ni kwamba Israel imeyashambulia maeneo ya kusini mwa Ukanda wa Gaza ambayo awali ilikuwa imetoa tahadhari kwa Wapalestina kuondoka kabla ya kufanya mashambulizi ya ardhini, na kuwaua watu kadhaa siku ya jumanne. Israel inadai kwamba inawalenga wanamgambo wa kundi la Hamas ambalo linatawala eneo hilo lililozingirwa.

Soma hapa: Hamas yampoteza kamanda wa ngazi za juu

Kukiwa hakuna maji, mafuta wala vyakula vinavyoingia Gaza tangu shambulizi baya dhidi ya Israel wiki iliyopita, wapatanishi wanajaribu kuondoa mkwamo huo ili angalau kufungua njia ya kusambaza misaada kwa raia walio na uhitaji, makundi ya misaada na hospitali. 

Kando na hayo, mapigano pia yamezuka katika mpaka wa Israel na Lebanon ambako kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran linaendesha shughuli zake. Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amewaonya wanamgambo wa Hamas kwamba wachague kufa ama wajisalimishe.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwasili IsraelPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

"Ndege zetu zinafika kila sehemu, ndege hii ina misheni nyingi lakini kila kombora lina anwani. Tutamfikia kila mwanachama wa Hamas. Wanachama wa Hamas wana machaguo mawili;  ama kufa katika nafasi zao au kujisalimisha bila masharti, hakuna chaguo la tatu. Tutalifuta shirika la Hamas na kulisambaratisha na uwezo wake wote, " alisema Gallant.

Marekani, na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani zinalitambua kundi la Hamas kuwa shirika la kigaidi.

Soma pia: Israel inasema Wapalestina 700,000 bado wapo kaskazini Gaza

Ama kwa upande mwingine pia wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, wameendelea kufurumusha maroketi katika miji kadhaa ya Israel leo Jumanne. Tahadhari ya maroketi imesikika katika miji ya kusini mwa nchi na kati karibu na mji wa pwani wa Tel Aviv. Wapiganaji wa Hamas walifanya shambulizi baya na la kushutukiza dhidi ya ya Israel Oktoba 7. Zaidi ya watu 1,400 wameuawa na takribani 4,000 wamejeruhiwa. Wanamgambo hao pia waliwateka watu wapatao 199 ikiwemo raia wa kigeni. Zaidi ya Wapalestina 2,800 wameuawa na zaidi ya 10,000 kujeruhiwa katika mashambulizi ya ulipizaji  kisasi ya Israel.

Taarifa zinasema kwamba Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz tayari ametua nchini humo katika ziara inayonuia kuonyesha mshikamano na Israel. Scholz atakutana na waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv kabla ya kuelekea Misri kukutana na Rais Abdel Fattah al-Sisi. 

Wakati hayo yakiendelea, Umoja wa Mataifa umeionya Israel hii leo dhidi ya "kuwahamisha kinguvu raia" katika Ukanda wa Gaza na kusema hatua hiyo inaweza kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa yake kwamba Israel ilikuwa na jukumu la kuhakikisha raia wanahamishwa kwa utaratibu ulio sawa kwa kuzingatia utaoji wa mahitaji muhimu na ya msingi lakini haikutimiza hilo.

Wapalestina wakipanga foleni kununua mikate kambi ya wakimbizi ya Rafah kusini mwa GazaPicha: Mohammed Abed/AFP

Kwingineko kuhusu mzozo huo ni kwamba jeshi la Marekani limeamuru askari wake wapatao 2,000 kujiandaa kwa ajili ya kupelekwa Mashariki ya Kati katikati mwa mvutano unaozidi kuongezeka baina ya Israel na kundi la Hamas huko Gaza. Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema kupelekwa askari katika eneo hilo utairuhusu Marekani "kushughulikia kwa haraka" mzozo huo. Tangazo hilo linatolewa wakati Ikulu ya Marekani ikisisitiza kwamba haikusudii kutuma vikosi vyake ndani ya Isreal. Naye Rais wa Marekani Joe Biden anajiandaa kuelekea Isreal ambako yeye na viongozi wengine wa ulimwengu wanajaribu kuepusha vita hivyo kuzua mzozo mkubwa wa kikanda.

Na kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameelezea mashambulizi ya Israel huko Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kutaka yakomeshwe mara moja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW