1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Jordan zafungua vivuko vya mpakani na Syria

15 Oktoba 2018

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamepita katika kivuko cha mpakani kilichofunguliwa tena kati ya eneo linalokaliwa na Israel la Milima ya Golani na Syria, kilichofungwa kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria.

UN Friedensmission Golan Höhen
Picha: Getty Images/J. Guez

Umoja wa Mataifa umesimamia ufunguzi wa kivuko cha Quneitra Jumatatu, kilichopo katika eneo la Milima ya Golan linalokaliwa na Israel. Kivuko hicho kilifungwa mwaka 2014 baada ya makundi ya waasi kuingia katika eneo hilo na kuwafurusha wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Vikosi vya Syria vililikamata tena eneo la Quneitra mwezi Julai.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisimamia makubaliano ya kujiondoa kwenye mapigano kati ya Israel na Syria tangu mwaka 1974. Jeshi la Israel limesema kivuko hicho kilichofunguliwa upya kitakuwa kinatumiwa tu na vikosi vya Umoja wa Mataifa.

"Kufunguliwa kwa kivuko hiki kunaashiria kuimsrishwa kwa makubaliano ya mwaka 1974 na kunaupa tena Umoja wa Mataifa uwezo wa kusimamia makubaliano hayo," alisema Meja Nehemia Berki, afisa anaehusika na mawasiliano kati kikosi cha kusimamia makubaliano ya kujiondoa kwenye mapigano cha Umoja wa Mataifa na jeshi la Israel.

Njia muhimu ya biashara na Jordan

Kivuko kingine muhimu kati ya Jordan na Syria kilifunguliwa pia leo, miaka mitatu baada ya eneo hilo muhimu la kibiashara kati ya mataifa hayo mawili kuangukia mikono mwa waasi na kusitisha usafiri.

Magari ya vikosi vya Umoja wa Mataifa vinavyosimamia makubaliano ya mwaka 1974 kati ya Syria na Israel.Picha: Getty Images/J. Marey

Kufunguliwa tena kwa kivuko hicho cha Nassib ni habari njema kwa serikali ya Syria, ambayo inalenga kutuma ujumbe kwa raia wake na dunia kwamba taratibu inaibuka mshindi katika vita vilivyoshuhudia umuagaji damu mkubwa, na inaanza kurejesha huduma muhimu na uhusiano.

'Tuko tayari kukomesha ugaidi Idlib'

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Syria amesema serikali iko tayari kuanzisha tena mashambulizi katika mkoa wa Idlib iwapo makubaliano yaliodikiwa kati ya Urusi na Uturuki hayatatekelezwa kama ilivyokubaliwa.

Waziri huyo Walid al-Moualem amesema hivi sasa ni juu ya Urusi kuamua iwapo makubaliano yalioepusha mashambulizi ya serikali dhidi ya ngome ya mwisho ya waasi katika mkoa wa Idlib yalikuwa yanatekelezwa, na kuogneza kuwa vikosi vyao viko tayari kwa kile alichokiita kuondoa ugaidi iwapo makubaliano hayaheshimiwi.

Kundi la waasi la Tahrir al-Sham ambalo ni muungano wa makundi ya wapiganaji wa jihadi linaloongozwa na tawi la zamani la kundi la Al-Qaeda, liliashiria siku ya Jumapili kuwa lingeheshimu masharti ya makubaliano hayo, ingawa halisema hilo bayana.

Mwandishi: iddi Ssessanga/rtre,afpe,aptn

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW