1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na kundi la Islamic Jihad wakubali kusitisha mapigano

Sylvia Mwehozi
8 Agosti 2022

Makubaliano "tete" ya usitishaji mapigano baina ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina yameonekana kufanya kazi mapema leo mjini Gaza na kuongeza matumaini ya kukomeshwa kwa mapigano ya karibu siku tatu.

Rauch steigt nach israelischen Luftangriffen im südlichen Gazastreifen auf
Picha: Ashraf Amra/ZUMA/IMAGO

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Misri ya usitishaji mapigano baina ya Israel na wanamgambo wa kundi la Kipalestina la Islamic Jihad PIJ katika ukanda wa Gaza, yalianza kufanya kazi saa tano na nusu usiku wa kuamkia Jumatatu baada ya pande zote kuridhia. Lakini dakika chache kabla ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano hayo, jeshi la Israel lilidai kuwalenga magaidi ndani ya Gaza, huku ving'ora vya mashambulizi ya anga vikisikika kusini mwa Israel. Soma Hamas yasema bado mapambano yanaendelea Gaza

Israel ilianza kufanya mashambulizi siku ya Ijumaa dhidi ya viongozi wa kundi la Islamic Jihad na kumuua kiongozi wa pili Khaled Mansour katika shambulio la anga kusini mwa Gaza Jumamosi jioni, pamoja na wanamgambo wengine wawili na raia watano.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa muda wa Israel Yair Lapid iliishukuru "Misri kwa juhudi zake" na ikathibitisha kuwa makubaliano hayo yataanza kutekelezwa, lakini ikaonya kwamba "ikiwa usitishaji vita utakiukwa, Israel inayo haki ya kujibu kwa nguvu." Kwa upande wake, kundi la Islamic Jihad nalo lilithibitsiha usitishaji mapigano lakini likaonya kwamba pia "linayo haki ya kujibu" uchokozi wowote.Tarek Selmi ni msemaji wa kundi hilo mjini Gaza na amethibitisha kufikiwa kwa makubaliano.

Maroketi yaliyorushwa kutokea upande wa GazaPicha: Bashar Taleb/ZUMA Wire/IMAGO

"Sasa kwa hakika tumefikia makubaliano na kuna dhamira ya Misri kusimamia kuachiliwa kwa wafungwa Khalil Awawda Na Bassam Al-Saadi haraka iwezekanavyo kutoka jela za Israel. Tunatangaza kusitisha mapigano ifikapo saa tano na nusu usiku na tunakaribisha juhudi za Misri ambazo zimefanywa kumaliza vita hivi."

Tangu Ijumaa, Israel ilifanya mashambulizi makali ya angani na mizinga katika maeneo ya kundi la Islamic Jihad mjini Gaza, huku wanamgambo nao wakirusha mamia ya makombora kulipiza kisasi.

Mbali na watu zaidi ya 40 waliouawa huko Gaza wakiwemo watoto 15, zaidi ya watu 300 wamejeruhiwa katika eneo la Palestina, ambalo linaendeshwa na kundi la Kiislamu la Hamas. Huduma za dharura zilisema kuwa watu watatu nchini Israel wamejeruhiwa huku wengine 31 wakijeruhiwa kidogo.Israel yashambulia kwa ndege za kivita Kusini mwa Gaza

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linapanga kufanya mkutano wa dharura hii leo juu ya ghasia hizo. China, ambayo inashikilia urais wa baraza hilo mwezi huu, imepanga mkutano huo kufuatia ombi la nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu, inayowakilisha mataifa ya kiarabu katika baraza hilo.

Kundi la Islamic Jihad lina wapiganaji na wafuasi wachache ukilinganisha na kundi la Hamas yamekuwa na vipaumbele tofauti, dhidi ya Israel.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW