1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Lebanon kufanya mazungumzo Washington

Josephat Charo
10 Aprili 2026

Afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema Israeli na Lebanon zitafanya mazungumzo mjini Washington wiki ijayo mjini Washington.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atalegeza mashambulizi Lebanon.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atalegeza mashambulizi Lebanon.Picha: Alex Brandon/AFP

Afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema Israeli na Lebanon zitafanya mazungumzo mjini Washington wiki ijayo, huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa kimataifa kwamba mashambulizi ya mabomu ya Israeli yanaweza kuuvunja mkataba wa kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran ambao tayari ni dhaifu.

"Tunaweza kuthibitisha kwamba Idara hiyo itaandaa mkutano wiki ijayo kujadili mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano na Israeli na Lebanon," afisa huyo wa Marekani alisema.

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu mapema Alhamisi alikuwa amewaamuru mawaziri wake kutafuta mazungumzo ya moja kwa moja na Lebanon, akilishinikiza kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran liweke chini silaha.

Lakini afisa wa serikali ya Lebanon aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba Beirut ilihitaji makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya kuanza mazungumzo yoyote na Israeli, siku moja baada ya mashambulizi makali kote nchini.

Israel na Lebanon hazijathibitisha hadharani kuhusu mazungumzo ya Marekani ya wiki ijayo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametaka mazungumzo na Lebanon.Picha: Ronen Zvulun/AFP/Getty Images

Hezbollah ilisema ilikuwa ikishiriki katika mapigano ya karibu dhidi ya vikosi vya Israeli ardhini kusini mwa Lebanon siku ya Alhamisi, huku mamlaka ya Lebanon wakisema mashambulizi ya Israeli yaliwaua watu wasiopungua 303 na kuwajeruhi 1,150 siku iliyopita.

Agizo la Netanyahu la mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Lebanon lililenga kuipokonya silaha Hezbollah na kuanzisha mchakato wa amani, kulingana na taarifa kutoka ofisini kwake, lakini hakutoa muda wa haraka wa kusitishwa kwa mashambulizi ya angani.

Mbunge wa Hezbollah baadaye alisisitiza tena kukataa mazungumzo yoyote ya moja kwa moja kati ya Lebanon na Israeli kwa kundi lake.

Trump ana matumaini na mazungumzo ya Islamabad

Wakati haya yakiarifiwa rais wa Marekani Donald Trump amesema ana matumaini makubwa kuhusu uwezekano wa kufikia makubaliano na Iran kabla ya mazungumzo yaliyopangwa wikendi hii huko mjini Islamabad nchini Pakistan. Alisisitiza kwamba Iran imeshindwa, akiongeza kwamba ikiwa hawatafanya makubaliano, hali itakuwa mbaya na ya uchungu sana.

Balozi wa Iran nchini Pakistan alifuta chapisho la mitandao ya kijamii akisema ujumbe wa Iran utawasili Pakistan siku ya Alhamisi. Afisa mmoja katika ubalozi wa Iran mjini Islamabad aliiambia AFP kwamba taarifa hiyo ilifutwa kwa sababu ya masuala fulani na akakataa kusema kama ujumbe huo bado ulikuwa unatarajiwa.

Ikiwa mazungumzo ya Pakistan yataendelea, hoja muhimu ya mzozo inabaki kuwa mlango bahari wa Hormuz, ambapo asilimia 20 ya mafuta duniani pamoja na kiasi kikubwa cha gesi asilia na mbolea hupitia.

Trump ameionya Iran kuhusu kutoza ushuru kwa meli zinazopita mlango bahari wa Hormuz.Picha: REUTERS

Trump aionya Iran kuhusu Hormuz

Trump ameionya Iran dhidi ya kuweka ushuru kwa meli zinazopita kwenye mlango bahari wa Hormuz akisema kwenye jukwaa lake la kijamii la Truth Social kwamba afadhali wasifanye hivyo na, ikiwa watafanya hivyo, afadhali waache sasa.

Starmer azungumza na Trump kuhusu kuufungua mlango bahari wa Hormuz

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu umuhimu wa mpango unaotekelezeka wa kuziwezesha meli kupitia mlango bahari wa Hormuz kufuatia usitishaji mapigano mashariki ya kati.

Hatua hiyo iInakuja huku Starmer akiwatembelea washirika katika eneo la Ghuba kwa mazungumzo kuhusu jinsi ya kuunga mkono kusitishwa kwa mapigano na kuhakikisha kufunguliwa tena kwa njia hiyo muhimu ya meli.

Anatarajiwa kurudi Uingereza Ijumaa baada ya kuziembelea Qatar, Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW