1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Israel na Lebanon zakubali masharti ya kusitisha vita

26 Novemba 2024

Israel inaonekana kuwa tayari kuukubali mpango wa Marekani wa kusitisha mapigano kati yake na kundi la wanamgambo la Hezbollah na hivyo kufungua njia ya kuvimaliza vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Lebanon | Beirut | Hezbollah
Wanajeshi wa Lebanon wakishika doria wakati zoezi la uokoaji likiendelea baada ya shambulizi la anga la IsraelPicha: Sally Hayden/SOPA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Vita hivyo vilichochewa na mzozo wa Gaza yapata miezi 14 iliyopita. Hayo yanaripotiwa wakati mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akisema Israel haina sababu ya kulikataa pendekezo hilo la kusitisha mapigano. 

Vyanzo vinne vya ngazi ya juu vya Lebanon vimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mpango huo wa Marekani utatoa fursa ya kutolewa tangazo rasmi la kusitisha mapigano litakalotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Soma pia: Wanamgambo wa Hezbollah warusha mkururo wa roketi Israel

Huko Mjini Washington, msemaji wa usalama wa kitaifa wa ikulu ya Marekani John Kirby alisema jana Jumatatu kuwa mpango huo wa kusitisha mapigano uko karibu kufikiwa wakati ofisi ya rais wa Ufaransa ikieleza kuwa majadiliano kuhusu mpango wa kusitisha mapigano yamepiga hatua kubwa.

Yaliyomo kwenye mpango wa kusitisha vita

Makubaliano hayo tayari yamepokewa kwa mikono miwili mjini Beirut, baada ya naibu spika wa Lebanon kusema kwamba njia ni nyeupe kwa makubaliano hayo kutekelezwa, labda tu iwapo Benjamin Netanyahu atabadilisha msimamo wake.

Hata hivyo, ofisi ya Waziri mkuu huyo imekataa kutoa kauli kuhusu ripoti kwamba Israel na Lebanon zimekubaliana juu ya mapendekezo yaliyotolewa na Marekani ya kusitisha mapigano.

Soma pia: Viongozi wa G20 watoa wito wa usitishwaji vita Gaza na Lebanon

Kundi la Hezbollah ambalo linachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Marekani, limemteua spika wa bunge la Lebanon Nabih Berri kuliwakilisha katika mazungumzo hayo.

Zoezi la uokoaji linaendelea baada ya shambulizi la anga la Israel lililolenga jengo la makaazi la orofa 8 eneo la Basta katikati mwa Beirut.Picha: Sally Hayden/SOPA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Mpango huo unapendekeza wanajeshi wa Israel kuondoka kusini mwa Lebanon huku wanajeshi wa Lebanon wakipelekwa katika eneo la mpakani, ambalo linachukuliwa kuwa ngome ya Hezbollah ndani ya siku 60.

Hata hivyo licha ya kuonekana dalili za kufikiwa kwa makubaliano hayo, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mashambulizi baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga na kusababisha uharibifu katika maeneo ya kusini mwa Beirut yanayodhibitiwa na Hezbollah.

Soma pia: HRW: Israel yalaumiwa kwa kutenda uhalifu wa kivita 

Uharibifu katika maeneo mengi ya Lebanon yameweka wazi changamoto inayowakadolea macho Walebanon ya kujenga upya makaazi yao huku zaidi ya watu milioni moja wakipoteza makaazi.

Lebanon imesema takriban watu 3,768 wameuawa nchini humo tangu Oktoba mwaka jana, wengi wao wakipoteza maisha wiki chache zilizopita, na kwa upande wa Israel, mamlaka imefahamisha kuwa wanajeshi 82 na raia 47 wameuawa.

Milipuko Beirut yasababisha maafa makubwa

01:17

This browser does not support the video element.

Ama kwa upande wa Israel, usitishaji mapigano utafungua njia kwa watu 60,000 kurejea makwao katika eneo la kaskazini baada ya kuyahama makaazi yao kutokana na kushadidi kwa mashambulizi ya angani ya Hezbollah.

Wakati hayo yanaarifiwa, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameitolea mwito serikali ya Israel kuunga mkono makubaliano yaliyopendekezwa ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah. Borell amefahamisha kuwa mapendekezo hayo yanatoa dhamana zote muhimu kwa usalama wa Israel.

Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa tajiri duniani G7 unaofanyika nchini Italia, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Ulaya amesema hakuna sababu za kutoutekeleza mpango huo wa makubaliano.

Ametaka Israel iwekewe shinikizo ili kuidhinisha makubaliano hayo mara moja.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW