1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISRAEL NA PALESTINA WAPATANA

8 Februari 2005

TAARIFA YA HABARI 16.00 08-02-05

SHARM EL SHEIKH:

Viongozi wa Israel na wa Mamlaka ya Ndani ya wapalestina wametangaza kukomesha rasmi mapigano ya umwagaji damu yaliodumu miaka 4 sasa.Hii inafuatia mkutano wa kilele huko Sharm El Sheikh leo hii kati ya waziri mkuu Ariel Sharon wa Israel na Kiongozi wa Palestina,Mahmoud Abbas.Sharon ametangaza kukomesha kuwahujumu wapalestina na wapalestina wameahidi kusimamisha hujuma zao dhidi ya waisraeli popote walipo.

Bw.Sharon akasema kuwa kwa mara ya kwsanza tangu kupita muda mrefu kuna matarajio katiukja eneo letu ya kuwa na mustakbala mwema tangu kwetu sisi hata kwa wajukuu zetu.

Pande hizi mbili lakini hazikutia saini makubaliano rasmi ya kusimamisha mapigano na Israel imesisitiza kwamba inashirikiana tu na Mamlaka ya Ndani ya wapalestina lakini sio na magaidi walio nyuma ya machafuko.

Machafuko yaliripuka hapo Septemba 2000 baada ya kuvunjika mazungumzo kuhusu ardhi zilizonyakuliwa na Israel mwaka 1967.Kiasi cha wapalestina 3,350 na waisraeli 970 wameuwawa katika kipindi hicho.

SHARM EL-SHEIKH:

Taarifa nyengine kutoka Sharm el-Sheikh zinasema, waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon, amemualika kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas kumtembelea shambani kwake katika Jangwa la kusini la Negev-hii ni kwa muujibu wa msemaji wa Bw.Sharon.

Alipoulizwa lini ,msemaji huyo alijibu karibuni hivi.Gissin alisema zaidi kuwa anatumai viongozi hawa wawili wanaweza pia kukutana mjini Ramallah,kituo cha utawala cha Mamlaka ya ndani ya wapalestina.

PARIS:

Waziri wa nje wa Marekani Bibi Condoleeza Rice amewasili hii leo mjini Paris, Ufaransa –shina la upinzani wa vita vya Iraq na akaarifu kuwa wakati umewadia kukomesha tofauti za zamani na kufungua ukurasa mpya katika ushirikiano kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya.

BAGHDAD:

Mshambulizi aliejitoa mhanga amejiripua katika mlolongo wa vijana waliokuwa katika mlolongo kujiandikisha kuwa wanajeshi hii leo na kuwaua watu 15 na kuwajeruhi wengine 13.

Watu waliojeruhiwa wamearifu jinsi gani mtu huyo aliejiripua akivaa ukanda wa miripuko alipowasili katika mlolongo huo wa watu waliotaka kujiandikisha jeshini.

Taarifa nyengine kutoka Baghdad zinasema vikosi vya Iraq vimemtia nguvuni jamaa wa rais Saddam Hussein alieondolewa madarakani ambae akigharimia waasi kwa fedha na kuwapatia silaha .Bashir Matar al-Tikritti alitiwa nguvuni Januari 13 katika mji wa Al-Sharqat uliopo kati ya anakotoka Saddam Tikrit na mji wa kaskazini wa Mosul.

Taarifa zasema kuwa Bashir akitiliwa shaka kuwapa kinga wajumbe waliosdakwa wa utawala wa zamani wa saddam pamoja na mtoto wake wa kiume Qusay kabla hakuuwawa Julai mwaka juzi.

GENEVA:

Viongozi wa Ulaya na wa Iran wameanza duru mpya ya mazungumzo mjini Geneva yenye shabaha ya kuondoa vizingiti vinavyozuwia mapatano kuhusu mradi wa kinuklia wa Iran.

Mazungumzo hayo yamewajumuisha pamoja mabingwa na maafisa kutoka Iran,Ujerumani,Uingereza na Ufaransa.

Iran inashikilia kwamba ina haki ya kutengeza nishati ya kinuklia wakati kambi ya magharibi inahofia Iran yaweza kuunda silaha za atomiki.

Iran imesimama wima katika dai lake kwamba haitaacha mradi wake wa kinuklia ikidai inauhitaji kujitosheleza na umeme.

NAIROBI:

Marekani imesimamisha kugharimia shuzghuli za kupiga vita rushua nchini Kenya .Hii inafuatia kujiuzulu kwa mkuu anaeongoza kampeni dhidi ya rushua akidai kuwa rais wa Kenya hakujitolea kweli kuondoa madhambi hayo.

Balozi wa Marekani nchini Kenya, akiarifu hatua hiyo ya kusimamisha kiasi cha dala milioni 2.5 kwa mwaka huu na ujao kwa vita dhidi ya rushua, alidai fedha hizo hazitatolewa hadi imepatijkana sura halisi juu ya nia hasa ya serikali ya Kenya.

Hatua hii imekuja siku moja baada ya mshauri mkuu wa rais Kibaki juu ya kupambana na rushua John Githiongo kujiuzulu.

LOME:

Chama cha Upinzani nchini Togo kimeitisha mgomo wa siku mbili wa kukaa nyumbani ili kulalamika kwa kuapishwa kuwa rais mpya mwana wa rais Eyadema aliefariki dunia jumam,osi iliopita.Faure Eyadema aliatawazwa rais wa Togo baada ya katiba ya nchi hiyo kurekebishwa.Baba yake Eyadema, alitawala Togo kwa kipindi cha miaka 37 mfululizo baada ya kunyakua madaraka kupitia mapinduzi ya wanajeshi.

Jumuiya ya Afrika magharibi ECOWAS imeitisha kesho kikao cha dharura kuizingatia hali ya mambo nchini Togo.Umoja wa Ulaya nao umeitaka Togo kuheshimu katiba.Na Umoja wa Afrika umeitishia Togo kuiwekea vikwazo.

HARARE:

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameonya kuwa Uingereza inajaribu kujenga nguzo yake ya ushawishi nchini Zimbabwe kupitia chama cha upinzani.Mugabe amemtuhumu waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kujiingiza katika uchaguzi wa Zimbabwe uliopangwa mwishoni mwa mwezi ujao,Machi 31.

COPENHAGEN:

Wananchi wa Danmark wamepiga kura hii leo kulichagua Bunge jipya.Matokeo ya awali yanabainisha kwamba serikali ya vyama vya mrengo wa kati na kulia ya waziri mkuu Anders Fogh Rasmussen yadhihirika itashinda tena kipindi cha pili cha utawala.

Kinaungwamkono na wadeni wengi kwa vita vyake vya kupambana na wanaomba ukimbizi nchini Danmark.