Israel na UAE kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia
14 Agosti 2020Israel na UAE zimekubaliana kurejesha mahusiano katika muafaka wa kihistoria, ambao ni wa tatu pekee wa aina hiyo ambao taifa hilo la Kiyahudi limewahi kusaini na taifa la Kiarabu, ambapo imeahidi kusitisha unyakuzi wa ardhi za Wapalestina.
Guterres amesema unyakuzi unaweza "ukafunga kabisa mlango" wa mazungumzo kati ya Israel na viongiozi wa Palestina na "kuharibu matumaini" ya kupatikana taifa la Kipalestina chini ya suluhisho la mataifa mawili. Waziri Mkuu wa Israel Bwenjamin Netanyahu amesema ni "siku ya kihistoria" na muafaka huo utafungua enzi mpya kwa ulimwengu wa Kiarabu na Israel. "Makubaliano haya ni pamoja na mahusiano kamili ya kidiplomasia, kufunguliwa kwa balozi na kubadilishana mabalozi, uwekezaji mkubwa ambao utaufaidi pakubwa uchumi wa Israel hasa wakati huu wa virusi vya corona, mahusiano ya kibiashara, utalii na safari za ndege zikiwemo za moja kwa moja kati ya Israel na Abu Dhabi."
Rais wa Marekani Donald Trump alisema viongozi wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu watasaini muafaka huo katika Ikulu ya White House katika kipindi cha karibu wiki tatu zijazo. Akizungumza baada ya mpango huo kutangazwa, Trump aliwasifu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Kiongozi wa UAE Sheikh Mohamed bin Zayed Al-Nahyan akisema ni washirika "wazuri zaidi" ambao wamedhihirisha "maono na uongozi bora".
Lakini Wapalestina wamepinga vikali mpango huo, wakiuita "usaliti" katika harakati zao, ikiwemo madai yao ya Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa lao la usoni. Rais Trump hata hivyo anahisi Wapalestina wataungana nao "Nadhani Wapalestina, watakuwa nasi hata bila kukiri sasa. Nadhani wanataka sana kuwa sehemu ya tunachokifanya. Na naona hatimaye amani kati ya Israel na Wapalestina -- naona hilo likifanyika. Nadhani wakati nchi hizi kubwa, zenye nguvu na tajiri zinaposhiriki, nadhani Wapalestina nao watafuata mkondo."
Mkutano huo wa kilele utarejesha kumbukumbu za utiaji saini wa awali katika Mashariki ya Kati nchini Marekani, ikiwemo Mikataba ya Olso mwaka wa 1993 ambayo ilimkutanisha mjni Washington aliyekuwa kiongozi wa Israel marehemu Yitzhak Rabin na kiongozi wa Wapalestina marehemu Yasser Arafat.
Rais Jimmy Carter pia alisimamia utiaji saini wa Mikataba ya Camp David kati ya Anwar Sadat wa Misri na Menachem Begin wa Israel mwaka wa 1978.
Rais Trump amedokeza kuwa UAE huenda isiwe nchi ya mwisho kufikia makubaliano na Israel ambayo mpaka sasa ilikuwa tu na mahusiano rasmi ya kidiplomasia na mataifa mengine mawili ya Kiarabu, Misri na Jordan.
Na saa chache tu baada ya Israel na UAE kutangaza mpango huo, Israel ikafanya mashambulizi ya angani yaliyoyalenga maeneo ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, wakati wiki ya uhasama kati ya Taifa hilo la Kiyahudi na ukanda huo wa Kipalestina ikiendelea. Israel imesema mashambulizi hayo, na hatua nyingine ikiwemo kusitisha usambazaji wa mafuta katika ukanda huo, ni ya kulipiza kisasi mabomu ya moto yaliyoning'inizwa kwenye maputo yanayoelea mpakani kutokea Gaza. Shambulizi hilo la usiku kucha kwenye maeneo yanayotumiwa na Hamas, kundi la itikadi kali linaloudhibiti ukanda huo, lilikuwa operesheni ya tano ya aina hiyo wiki hii.
afp, dpa, reuters, ap