1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Serikali mpya yatarajiwa kuapishwa

13 Juni 2021

Waziri Mkuu mtarajiwa wa Israel Naftali Bennett amesema itakuwa makosa kufufua mkataba wa kimataifa wa silaha za nyuklia wa Iran.

Israel Bennett und Netanjahu in der Knesset
Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Katika hotuba yake bungeni, Bennett amesema Israel itaendelea kuwa tayari kuchukua hatua dhidi ya Iran.

"Israel haitairuhusu Iran kujihami kwa silaha za nyuklia. Israel haitakuwa mshirika wa makubaliano hayo na itaendelea kulinda uhuru kamili wa kuweza kuchukua hatua," amesema Bennett.

Kauli hizo kali zinaendeleza sera za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu za kuikabili Iran.

Soma pia: Bunge la Israel kuipigia kura serikali mpya

Bennett pia alimshukuru Rais Biden na utawala wake kwa kuiunga mkono Israel kwa miongo mingi.

Serikali mpya ya Bennett inatarajiwa kuapishwa baadaye Jumapili baada ya kura bungeni.

Uapisho huo utamaliza utawala wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 12 na hivyo atakuwa upande wa upinzani.

Mkwamo wa kisiasa Israel

Benjamin Netanyahu amekuwa waziri Mkuu wa Israel kwa miaka 12 iliyopitaPicha: XinHua/dpa/picture alliance

Israel imekuwa katika mkwamo wa kisiasa kwa miaka miwili baada ya kufanya chaguzi nne lakini bila ya mshindi wa wazi kupatikana.

Naftali Bennett, kiongozi wa chama kidogo chenye misimamo mikali, atachukua usukani kuwa waziri mkuu. Lakini ikiwa anataka kuendelea na wadhifa huo, ni lazima aendeleze ushirikiano usio wa kawaida kwenye muungano wao na vyama vingine vya mirengo ya kulia, shoto na kati.

Vyama vinane kikiwemo chama kidogo cha Kiarabu ambacho kimeweka historia kwa kushirikishwa kwa mara ya kwanza nchini humo kwenye muungano unaotawala vimeungana katika upinzani wao dhidi ya Netanyahu na dhidi ya uchaguzi mpya. Hata hivyo vyama hivyo vinatofautiana kuhusu mambo mengi.

Muungano mpya dhidi ya Netanyahu utadumu?

Mbunge nchini Israel Betzalel Smotrich akitupa cheche za maneno bungeni Juni 13, 2021 wakati serikali mpya ikitarajiwa kuapishwaPicha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Vyama hivyo vinatarajiwa kutafuta mkakati wa kupunguza msuguano na Wapalestina na vilevile kuendeleza uhusiano mzuri na Marekani bila ya kuanzisha miradi mikubwa mipya.

Netanyahu ambaye anakabiliwa na madai ya ufisadi, anaendelea kuwa mkuu wa chama kikubwa zaidi katika bunge la Israel na anatarajiwa kupinga vikali serikali hiyo mpya.

Endapo chama kimoja tu kitajiondoa, basi muungano huo unaweza kupoteza wingi na kuwa katika hatari ya kusambaratika, hivyo kumpa Netanyahu nafasi nyingine ya uwezekano wa kurudi madarakani.

(AP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW