1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Tunayo fursa kuishambulia miradi ya nyuklia ya Iran

12 Novemba 2024

Israel imesema kwa sasa iko katika nafasi nzuri ya kuweza kufikia malengo yake ya kushambulia miundombinu ya nyuklia ya Iran na hivyo kuondoa kabisa kitisho kwa taifa hilo.

Mfanyakazi akiendesha baiskeli karibu na kinu cha nyuklia cha Bushehr nchini Iran
Mfanyakazi akiendesha baiskeli karibu na kinu cha nyuklia cha Bushehr nchini IranPicha: Majid Asgaripour/AP/picture alliance

Kauli hiyo imetolewa na Waziri mpya wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, ambaye amedokeza kuwa Israel kwa sasa inayo "fursa" ya kuilenga miundombinu ya nyuklia ya Iran ambayo amesema kwa sasa iko katika hatari ya kushambuliwa.

Hata hivyo, Mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia IAEA Rafael Grossi ametahadharisha kuwa kwa sasa Iran inayo madini ya kutosha ya urani yaliyorutubishwa hadi kufikia viwango vya kuweza kutengeneza mabomu kadhaa ya nyuklia ikiwa itaamua kufanya hivyo. Madai yanayokanushwa na Tehran inayosema kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa kiraia na wenye lengo la amani.

Waziri mpya wa ulinzi wa Israel, Israel KatzPicha: MENAHEM KAHANA/AFP

Katz ambaye ameteuliwa hivi karibuni kushikilia wadhifa huo wa Waziri wa ulinzi wa Israel, amewaambia maafisa wa kijeshi kwamba hakutakuwa na mpango wa usitishwaji mapigano na kundi la Hezbollah na badala yake kundi hilo litaendelea kushambuliwa kwa nguvu zote.

Soma pia: Mkuu wa Shirika la kudhibiti nyuklia kuizuru Iran hivi karibuni

Hayo yakiarifiwa, mashambulizi makali ya Israel yameripotiwa kuyapiga maeneo yanayojulikana kama ngome za Hezbollah katika vitongoji vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Taarifa zinaeleza kuwa serikali mjini Tel-Aviv imeamuru mashambulizi hayo baada ya kuwataka raia kuondoka maeneo hayo.

Jeshi la Israel limeyalenga maeneo ya Haret Hreik, Ghobeiri, al Hadath, Beir al Abed na Lailaki. Mashambulizi hayo mazito ya anga yalisababisha hofu miongoni mwa raia wa Lebanon ambao baadhi walijielekeza haraka mashuleni kuwachukuwa watoto wao.

Ukanda wa Gaza washambuliwa pia

Haya yanajiri wakati mamlaka ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema takriban watu 37 wameuawa hivi leo kufuatia mashambulizi ya Israel katika ardhi ya Palestina. Pia, jeshi la  Israel limesema wanajeshi wake wanne wamefariki katika mapigano kaskazini mwa Gaza.

Raia wa Palestina wakiwa na huzuni baada ya mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Omar AL-QATTAA/AFP

Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza ambako kumekuwa kukiripotiwa matatizo ya uhaba wa misaada. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema Wapalestina wanapoteza matumaini kutokana na shehena ya misaada kuzuiliwa kuingia katika eneo la kaskazini mwa Gaza.

Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza na lebanon

Louise Wateridge, ni Afisa Mwandamizi wa masuala ya Dharura wa UNRWA:

" Msaada unaoingia Ukanda wa Gaza uko katika kiwango cha chini kabisa kwa miezi kadhaa. Wastani wa mwezi wa Oktoba ulikuwa lori 37 kwa siku katika Ukanda wote wa Gaza. Na ninaweza kukuambia, hiyo ilikuwa ni kwa watu milioni 2.2."

Hata hivyo Israel imesema inaendelea kuwezesha usafirishaji wa misaada zaidi kuelekea Gaza kabla ya kukamilika kwa muda wa mwisho wa siku 30 uliotolewa na Marekani.

(DPA,AP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW