1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yaacha uharibifu ´usio mfano´ hospitali ya Al Shifa

1 Aprili 2024

Vikosi vya Jeshi la Israel vimeondoka kutoka hospitali ya Al Shifa iliyo Ukanda wa Gaza ikiacha nyuma uharibifu usio mfano wa majengo na miili ya Wapalestina ikiwa imetapakaa kwenye uchafu.

Mabaki ya hospitali kubwa ya Al Shifa ya Ukanda wa Gaza
Mabaki ya hospitali kubwa ya Al Shifa ya Ukanda wa GazaPicha: AFP/Getty Images

Mamia ya watu, ikiwemo wale waliokuwa wanajihifadhi kwenye hospitali hiyo kubwa zaidi kwenye Ukanda wa Gaza kabla ya uvamizi wa jeshi la Israel, walimiminika kwenye majengo yake kutizama uharibifu uliofanywa na kuokota okota vitu walivyoviacha nyuma.

Jeshi la Israel limesema limewaua au kuwatia nguvuni mamia ya wanamgambo wa Hamas kwenye hospitali hiyo, na kudai pia limekamata silaha na nyaraka za kijasusi. Limearifu pia kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa wakati wa mapigano.

Limesema vilevile kwenye operesheni hiyo askari wake walijaribu kuepusha madhara kwa raia, wagonjwa na wafanyakazi wa huduma za afya.

Hata hivyo madai ya kukamatwa au kuuliwa wanamgambo wa Hamas kwenye hospitali hiyo yanakanushwa na kundi hilo na madaktari.

Kundi la Hamas lasema jeshi la Israel limefanya mauaji makubwa 

Makaburi ya Wapalestina kwenye hospitali ya Al Shifa Picha: Mohammed Ali/Xinhua/picture alliance

Ofisi ya idara ya habari inayoongozwa na kundi la Hamas imesema wanajeshi wa Israel wamewaua Wapalestina 400 kwenye hospitali ya Al Shifa akiwemo daktari mwanamke na mtoto wake wa kiume ambaye pia ni daktari.

Pia imelilaumu jeshi la Israel kwa operesheni yake iliyosababisha kusitishwa kwa huduma za afya kwenye hospitali hiyo iliyokuwa ikitegemewa na maelfu ya wakaazi wa Gaza.

"Mkoloni ameharibu na kuchoma moto majengo yote ndani ya Al Shifa. Wametifuatifua eneo lote la nje, na kuwafukia kwa vifusi miili ya watu waliowaua, na kuligeuza eneo hilo kuwa kaburi la halaiki," amesema Ismail Al-Thawabta, mkurugenzi wa idara ya habari ya Hamas.

"Huu ni uhalifu dhidi ya ubinadaamu," ameongeza afisa huyo alipozungumza na waandishi habari.

Msemaji wa Huduma za Dharura kwenye Ukanda wa Gaza amesema vikosi vya Israel viliwanyonga watu wawili ambao miili yao imepatikana kwenye eneo la hospitali ikiwa imefungwa pingu, na wakatumia matingatinga kuchimbua eneo la hospitali kitendo kilichofukua pia maiti zilizokwishazikwa.

Shirika la Habari la Reuters halikuweza kuthibitisha taarifa hizo na jeshi la Israel halikupatikana mara moja kujibu hata lilipoombwa kufanya hivyo.

Mkaazi asema hakuna kilichosalia baada ya wanajeshi kuondoka

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, ambayo haikuweza kuthibitishwa mara moja na shirika la habari la Reuters,  imeonesha maiti, baadhi zikiwa zimefunikwa kwa blanketi, zimetapakaa kwenye jengo kuu la hospitali, ambalo kwa sehemu kubwa kuta zake zimesambaratishwa.

Zimeonesha pia ardhi imetifuliwa, majengo mengine kadhaa yameharibiwa kabisa au kuchomwa moto.

"Sijaacha kulia tangu nilipofika hapa, mauaji makubwa yamefanywa hapa na dola hii kandamizi," amesema Samir Basel  43, alipozungumza na Reuters kupitia ujumbe mfupi wakati alipokuwa amefika kuitembelea hospitali ya Al Shifa.

"Eneo limeharibiwa, majengo yamechomwa moto na kuharibiwa. Eneo hili yafaa lijengwe upya - kwa maana hakuna tena hospitali ya Al Shifa."

Wapalestina walifika kukagua mabaki ya hospitali ya Al Shifa baada ya vikosi vya Israel kuondoka.Picha: AFP/Getty Images

Video nyingine iliopatikana na Reuters inaonesha Wapalestina wakirejea kwenye viunga vya hospitali hiyo kukusanya magodoro na vitu vingine walivyovitelekeza wakati vikosi vya Israel vimeivamia.

Sehemu kubwa ya vitu hivyo walivyokuwa wakivitumia walipokuwa wanajihifadhi kwenye majengo ya hospitali vimeharibiwa au vimefunikwa na vifusi.

"Tuliondoka tukitumai tutarudi na kukuta vitu vyangu. Hakuna hata kilichosalia. Nyumba yangu imepigwa bomu na kila kitu kimepotea. Sina nilichobakiwa nacho," amesema mwanamke mmoja.

"Nimekwenda kutafuta eneo la kujihifadhi kwenye shule moja lakini nimeambiwa hakuna nafasi, Niende wapi?"

Marekani na Israel kujadili mpango wa uvamizi wa ardhini wa mji wa Rafah

Mamia kwa maelfu ya watu wamekwama kwenye mji wa Rafah baada ya kukimbia mapigano maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.Picha: AFP/Getty Images

Wakati hayo yakiripotiwa Israel na Marekani zinafanya mazungumzo kuhusu mpango wa uvamizi wa ardhini wa vikosi vya Israel kwenye mji wa Rafah.

Mazungumzo hayo yatafanyika kwa njia ya mtandao wiki moja baada ya Israel kuifutilia mbali safari iliyokuwa imepangwa ya kwenda mjini Washington.

Mivutano kati ya washirika hao wawili imeongezeka kutokana na idadi kubwa ya vifo vya raia vinavyoshuhudiwa Ukanda wa Gaza.

Na mashaka yamekuwa makubwa zaidi mjini Washington juu ya dhamira ya Israel ya kutaka kufanya operesheni ya kijeshi kwenye mji uliofurika watu wa kusini mwa Gaza wa Rafah.

Israel ilikubali kutuma ujumbe wake kwenda Marekani kwa mashauriano kuhusu mpango huo, lakini ziara hiyo ilifutwa baada ya Marekani kutotumia kura yake ya turufu kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotoa mwito wa kusitishwa vita vya Gaza. Marekani iliamua kujizuia kulipigia kura azimio hilo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW