1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaadhimisha miaka 70 tangu kuundwa kwake

Sylvia Mwehozi
19 Aprili 2018

Israel imeanza maadhimisho ya kutimiza miaka 70 tangu kuundwa kwake ambapo waziri mkuu wa taifa hilo Benjamin Netanyahu ametumia maadhimisho hayo kuwaonya maadui zake na kugusia mahusiano na baadhi ya mataifa ya kiarabu.

Israel Jerusalem Feier Unabhängigkeitstag
Picha: Reuters/R. Zvulun

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu amezindua maadhimisho ya uhuru wa Israel usiku wa jana Jumatano katika sherehe za kuwasha mwenge, na kutoa vitisho kwa Iran pamoja na kutoa mkono wa mshikamano kwa wale wanaotaka amani.

Natanyahu amesema Israel inakabiliwa na kuendelea kwa uchochezi kutoka kwa jirani zake, ambao wengi wanakataa kukubali na uwepo wa taifa hilo na kuonya kwamba "yeyote atakayeinua mkono dhidi yetu hatosamehewa".

Pia Netanyahu hakusita kuusifu uamuzi wa rais Donald Trump alioutoa mapema mwaka huu kuhusu Israel akisema kuwa, "wote tunausifu uamuzi wa kihistoria wa Rais Donald Trump wa kuitambua Jerusalem kama mji wetu mkuu na kuuhamisha ubalozi wa taifa lenye nguvu duniani. Asante sana rais, asante sana Marekani."

Mvutano na majirani zake 

Wakati huo huo pia waziri mkuu Netanyahu alisema wanawakaribisha kwa mikono miwili majirani zake wote wanaotaka amani. Kauli ya Netanyahu inakuja wakati mvutano na Iran unaongezeka juu ya uwepo wake nchini Syria na ishara kwamba uadui wa miongo kadhaa baina ya Israel na mataifa ya kiarabu ya Ghuba unarudi juu ya wasiwasi wa pamoja kuhusu Iran.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Getty Images/AFP/D. Hill

Netanyahu amerejelea vitisho dhidi ya Iran iliyojiingiza Syria iliyokumbwa na vita, na kuonya kwamba Israel haitasita kujitetea yenyewe. Wasiwasi unaongezeka juu ya uwezekano wa vita ya kikanda baina ya Israel na Iran.

Mapema wakati wa sherehe za kuwakumbuka askari waliopoteza maisha na waathirika wa ugaidi, Netanyahu alizungumzia juu ya "ukatili wa uasi wa itikadi kali za Kiislamu". Kuwashwa kwa mwenge kunazindua maadhimisho ya uhuru yanayojumuisha sherehe, matamasha na urushaji wa fataki.

Rais wa Marekani Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amemtakia Netanyahu na Israel maadhimisho mema ya miaka 70 na kusema anatazamia kuuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem mwezi ujao.

Mipango ya kuuhamisha ubalozi imewatia hasira Wapalestina na ulimwengu wa kiislamu, na kuondosha matumaini ya kuyafufua tena mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina kuelekea ufumbuzi wa mataifa mawili.

Waandamanaji wa Kipalestina wakidondosha fensi katika ukanda wa GazaPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Hamra

Maandamano ya Wapalestina

Maadhimisho ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa taifa la kiyahudi yanakuja mnamo Israel ikikabiliwa na maadamano ya Ijumaa kila wiki yanayofanywa na wapalestina huko Gaza. Vikosi vya Israel viliwaua Wapalestina 34 na kuwajeruhi wengine kadhaa tangu maandamano hayo yalipoanza Machi 30.

Israel inaishutumu Hamas kwa kuratibu maandamano. Hapajakuwa na majeruhi kwa upande wa Isael.

Waandaaji wa Kipalestina wamesema mfululizo wa maandamano hayo makubwa kuanzia machi 30 hadi Mei 15, kumbukumbu ya miaka 70 ya "Nakba" au "janga" wakati Wapalestina 750,000 walipolazimishwa kuondoka katika makazi na ardhi yao na majeshi ya Israel mwaka 1948.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DW

Mhariri: Josephat Charo