Israel yaanzisha upya mashambalulio dhidi ya Gaza
8 Januari 2009Wanajeshi wa Israeli wameanzisha upya mashambulio baada ya kumalizika saa tatu za utulivu kutoa nafasi kwa misaada ya kiutu kuingia Gaza.
Misaada ya mbali mbali iliingizwa Gaza hapo jana wakati wa kipindi hicho .Hatua ya Israeli ya kusimamisha vita kwa saa tatu kila siku imepongezwa na mashirika ya kutoa misaada katika Gaza.
John Ging mkuu wa shirika la misaada la Umoja wa mataifa UNRWA anasema wameridhia hatua hiyo kama hatua ya kwanza ingawa sio suluhisho na pia wanatumai kwamba itakuwa ni muda wa saa tatu utakaotoa usalama kwa watu milioni moja na nusu wa Gaza.
Kwa upande mwingine juhudi za kidiplomasia zinaendelea lakini baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeshindwa kukubaliana juu ya hatua ya kumaliza mzozo huo lakini Marekani imetangaza kuunga mkono mpango uliopendekezwa na Misri na Ufaransa wa kusitisha mapigano.
Misri itaandaa mazungumzo na pande zote mbili Israel na Hamas juu ya pendekezo hilo.Ujerumani pia imekubaliana na pendekezo la rais Hosni Mubarak juu ya kusimamishwa vita kati ya Hamas na Israeli.
Aidha waziri wa mambo ya nje Frank Walter Steinmeir amepongeza hatua ya Israeli ya kutoa nafasi ya kupelekwa misaada ya kiutu katika ukanda wa Gaza.
Kwa upande mwingine wanasiasa wa ngazi ya juu kutoka vyama vyote vya serikali ya muungano wameonyesha nia ya kuridhia jeshi la kuweka amani la Ujerumani kulinda amani Gaza ikiwa kutafikiwa makubaliano ya kusitisha vita chini ya azimio la Umoja wa mataifa.
Hata hivyo msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema kuwa ni mapema mno kuzungumzia suala hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za hospitali katika Gaza watu zaidi ya 700 wameuwawa na wengine 3000 wamejeruhiwa hadi sasa tangu Israeli ilipoanzisha mashambulio dhidi ya Hamas.