1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaapa kujibu iwapo Iran itashambulia

12 Aprili 2024

Jeshi la Israel limesema limejitayarisha kuilinda nchi hiyo na kujibu mapigo iwapo Iran itafanya mashambulizi ya kulipa kisasi kutokana na hujuma iliyolilenga jengo lake la ubalozi nchini Syria.

Israel
Vifaru vya kijeshi kutoka Israel Picha: Jack Guez/AFP

Watawala mjini Tehran wameitwika dhima Israel ya kuhusika na shambulizi hilo lililofanywa na ndege za kivita mnamo Aprili 1 kwenye ubalozi mjini Damascus na tangu wakati huo wameapa kwamba Iran italipa kwa kilichotokea. Kwenye shambulio hilo ambalo Marekani pia inaamini lilifanywa na Israel, makamanda wawili na makuruta wengine kadhaa wa jeshi la Iran waliuawa.

Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha Iran

Katika siku za karibuni Israel na Marekani zimekuwa kwenye hali ya juu ya tahadhari, zikiamini kwamba Iran inapanga kufanya mashambulizi kujibu kisa cha mjini Damascus. 

Awali mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo mbili walizungumza kwa njia ya simu kujadili mashaka yaliyopo na kwa pamoja wamekubaliana kuvikabili vitisho kutoka dola hiyo ya Uajemi.