Israel yabomoa makaazi ya mpalestina aliyewashambulia
19 Novemba 2014Waumini wa kiyahudi wamerejea kusali katika sinagogi hilo lililoshambuliwa hapo jana na wapalestina wawili ambao waliwaua watu wanne na askari mmoja kwa kutumia bunduki na mashoka.Mmoja wa waumini hao Gavriel Cohen amesema shambulizi hilo la jana linaonyesha kuwa hatma yao ya baadaye inategemea mapenzi ya mwenyezi Mungu.
Waziri mkuu wa Israel ameapa kuchukua hatua kali kukabiliana na ongezeko la visa vya mashambulizi kutoka kwa wapalestina yanayowalenga waisrael.Na siku moja baada ya tamko hilo, maafisa wa usalama wa Israel wamebomoa nyumba ya mpalestina aliyewaua watu watatu mwezi uliopita katika shambulizi lililowalenga abiria waliokuwa wakisubiri kuabiri treni kituoni mjini Jerusalem.
Waumini wa kiyahudi warejea kusali
Jeshi na polisi la Israel limetoa taarifa inayosema wameyabomoa makaazi ya Abdel Rahman Shaloudi leo alfajiri. Shaoludi kijana wa umri wa miaka 21 aliuawa na askari alipokuwa akijaribu kutoroka baada ya kuwagonga kwa gari lake abiria kituoni.
Ghasia zimeongezeka mjini Jerusalem na maeneo mengine nchini Israel tangu mwezi Julai kufuatia kuchomwa hadi kuuawa kwa kijana wa kipalsetina na washambuliaji wa kiyahudi na baadaye mashambulizi ya kulipiza kisasi yakasababisha vifo vya vijana watatu wa kiisrael yaliyosababisha Israel kuushambulia kwa ukanda wa Gaza kwa siku hamsini.
Jeshi la Israel lilikuwa likibomoa au kuripua makaazi ya wanamgambo kwa miongo kadhaa lakini liliacha mwaka 2005 kwa kugundua haikuzuia mashambulizi dhidi ya Israel lakini limerejea kuzibomoa nyumba za washambuliaji kama njia ya kuwaadhibu washambuliaji na jamaa zao.
Netanyahu ameahidi kuharakisha ubomoaji wa makaazi ya washambuliaji waliofanya mashambulizi yote ya hivi karibuni mjini Jerusalem kuambatana na sera iliyoanzishwa tena mapema mwezi huu.
Ubomoja ni ukiukaji wa haki za kimataifa
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani sera hiyo ya Israel kama adhabu inayowalenga sio tu washambuliaji bali familia zao ambao hawana hatia. Shirika la Amnesty International limesema kuziboma nyumba za familia za washambuliaji ni ukiukaji wa haki za kimataifa.
Shambulizi la jana katika sinagogi ndilo baya zaidi kuwahi kushuhudiwa mjini Jerusalem tangu mwaka 2008 ambapo mpalestina aliyekuwa na bunduki aliwaua watu wanane katika shule ya kidini.
Palestina inaitaka Israel kuikabidhi maeneo ya Jerusalem,ukanda wa Gaza na ukingo wa magharibi maeneo yaliyonyakuliwa na Israel baada ya vita vya mwaka 1967.
Huku hayo yakijiri, bunge la Uhispania hapo jana jioni lilipiga kura kwa wingi kutaka Palestina kutambuliwa kama taifa huru.Wabunge 319 dhidi ya wawili walipiga kura kuitambua Palestina na kuitaka serikali ya waziri mkuu Mariano Rajoy kuitambua rasmi Palestina kwa kusema hiyo ndiyo suluhisho pekee ya kuumaliza mzozo wa mashariki ya kati.
Mwandishi:Caro Robi/ap/afp/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman