Israel yaendelea kuihujumu Gaza
11 Julai 2014Zaidi ya wapalastina 80 wameuuliwa tangu jumanne iliyopita katika eneo hilo linalozingirwa,wengi wao ni raia.Madege ya Israel yameushambulia alfajiri ya leo mji wa Gaza na ule wa Rafah na kuangamiza maisha ya watu wasiopungua wanne.
Kombora la wanamgambo wa kipalastina limepiga katika kituo cha kuuza mafuta katika mji wa Israel wa Ashdod na kusababisha mripuko mkubwa na kuwajeruhi watu wasiopungua watatu.
Jeshi la Israel limesema wanaanga na wanamaji wamehujumu vituo kadhaa bila ya kutoa maelezo zaidi.Kwa jumla jeshi la Israel linasema limehujumu vituo 860 katika Ukanda wa Gaza.
Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni jana usiku waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema:" Tumewapiga Hamas na magaidi na kwa wakati wote ambao kampeni hii inaendelea tutaendelea kuwahujumu."
Ameshadidia waziri mkuu wa Israel aliyepuuza pendekezo la rais Barack Obama la kutaka kupatanisha.
Katika mazungumzo ya simu kati ya rais Barack Obama na waziri mkuu wa Israekl Benjamin Netanyahu,rais Obama alisema Marekani iko tayari kurahisisha kuondowa uhasama ikiwa ni pamoja na kurejeshwa makubaliano ya kuwekwa chini silaha yaliyofikiwa Novemba mwaka 2012.
Wapalastina wanaasema hawatoondoka
Katika wakati ambapo Israel inatishia kutuma vikosi vya nchi kavu waziri wa ulinzi Moshe Yaalon anasema wanajiandaa kwa mapambano ya muda mrefu kutokana na kuzidi kufyetuliwa makombora na Hamas.
Makombora matatu yaliyofyetuliwa kutoka Gaza yameteketezwa na mtambo wa kukinga hujuma za makombora Iron Dome,huko Tel Aviv. Na kombora lililofyetuliwa toka kusini mwa Libnan limepiga kaskazini ya Israel lakini bila ya kusababisha hasara yoyote.
Hujuma za mabomu ya Israel hazijafanikiwa hadi sasa kukomesha makombora ya Hamas.
Msemaji wa Hamas huko Gaza,Sami Abou Zouhri anasema tunanukuu:" tumebanwa,hatuna cha kupoteza.
Kwa upande wake kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina mahmoud Abbas anasema:"Wanataka tuihame nchi yetu,lakini hatutoondoka.hatuna silaha,lakini tutapigana kwa kutumia macho yetu,tutapigana kwa maneno".
Israel yaadhibu waaliomo na wasiokuwemo
Misri pia imelaani "mtindo wa Israel wa kuwaadhibu waliomo na wasiokuwemo na kuitolea wito jumuia ya kimataifa ikomeshe haraka ugonvi huu ulioangamiza maisha ya karibu watu 100 haadi sasa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu