1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yaendelea na mashambulizi Gaza

9 Desemba 2023

Israel yashambulia maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza siku ya Jumamosi baada ya Marekani kuzuia jitihada zisizo za kawaida za Umoja wa Mataifa za kusitisha mapigano.

Gazastreifen | Zerstörungen durch den anhaltenden Krieg
Picha: Amir Levy/Getty Images

Wafanyakazi wa misaada wanasema mfumo wa huduma za kibinadamu wa Gaza unaelekea kuporomoka, huku kukiwa na kitisho cha magonjwa na njaa. Kura ya turufu ya Marekani kwenye Umoja wa Mataifa ililaaniwa na Mamlaka ya Palestina na Hamas, ambayo wizara ya afya imesema idadi ya vifo Gaza inafikia 17,490, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Shambulio la anga la Israel katika mji wa kusini wa Khan Yunis liliua watu sita, huku wengine watano wakiuwawa katika shambulio tofauti mjini Rafah, wizara hiyo ilisema Jumamosi.

Wizara ya afya ya Gaza imeongeza kuwa, katika kipindi cha saa 24, watu 71 wameuawa na wengine 160 kujeruhiwa. Majerehi walipekwa katika hospitali ya Al-Aqsa huko Deir al-Balah baada ya mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu. Milio ya risasi ilisikika katika wilaya ya jiji hilo ya Al-Zawaida.

Kikosi cha Ezzedine al-Qassam Brigedi, mrengo wenye silaha wa kundi Hamas, kilisema kilirusha makombora Jumamosi kuelekea Reim kusini mwa Israel, ambapo watu wenye silaha wa Hamas waliwauwa watu 364, katika tamasha la muziki Oktoba 7.

Misimo ya Israel na Marekani kwenye Umoja wa Mataifa

Mataifa ya kiislamu yaitaka Marekani kuishikiza Israel kusitisha mapigano GazaPicha: Mohammed Abed/AFP

Maeneo makubwa ya Gaza yameharibiwa na kuwa vifusi na Umoja wa Mataifa unasema takriban asilimia 80 ya watu wameyakimbia makazi yao, huku kukiripotiwa uhaba mkubwa wa chakula, mafuta, maji na dawa.

Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alishinikiza kura ya nadra ya Baraza la Usalama kwa kutumia hatua ambayo haijatumika kwa miongo kadhaa. Guterres alitaka baraza liidhinishe usitishaji mapigano kwa sababu, alisema, hali inayozidi kuzorota kwa kasi inafanya "kutowezekana kwa operesheni za maana za kibinadamu", kukiwa na athari zisizoweza kupewa ufumbuzi kwa amani na usalama wa kikanda.

Marekani siku ya Ijumaa ilipinga azimio la Baraza la Usalama. Mjumbe wa Marekani Robert Wood alisema azimio hilo "limetalikiana na hali halisi" na "litaiacha Hamas iweze kurudia kile ilichofanya Oktoba 7".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen alisema usitishaji vita "utazuia kutokomezwa" kwa Hamas "ambayo inatekeleza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, na itaiwezesha kuendelea kutawala Ukanda wa Gaza".

Marekani yakosolewa 

Rais wa Uturuki, Reccep Tayip Erdogan aomba mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: CHARLY TRIBALLEAU/AFP/Getty Images

Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas alisema "anaishikilia Marekani kuwajibika kwa umwagaji damu wa watoto, wanawake na wazee wa Kipalestina" huko Gaza baada ya kura ya turufu ya Marekani.

Avril Benoit, mkuu wa shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka,MSF, alielezea kura ya turufu ya Marekani kama "tofauti kubwa na maadili ambayo inadai kuwa inazingatia".

Rais wa Uturuki, Reccep Tayip Erdogan alikosoa vikali hatua ya Marekani na kuomba mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kundi la Hamas lilishutumu kura ya turufu kama "ushiriki wa moja kwa moja wa uvamizi katika kuua watu wetu". Iran, ambayo inaunga mkono Hamas, ilionya kuhusu uwezekano wa "mlipuko usioweza kudhibitiwa katika eneo hilo'' baada ya hatua ya Marekani.

Watu wengi miongoni mwa wa Gaza milioni 1.9  waliokimbia makazi yao kutokana na vita wameelekea kusini mwa Ukanda wa Gaza, na kuifanya Rafah karibu na mpaka wa Misri kuwa kambi kubwa ya wakimbizi.  

 

Vyanzo: AFP na Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW