1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Saleh Mwanamilongo
17 Januari 2024

Jeshi la Israel limesema limemuua mwanamgambo wa ngazi ya juu wa Kipalestina katika shambulio la anga katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.

Vita vya Gaza| Khan Younis
Jeshi la Jordan lasema hospitali yake ya dharura katika mji wa Khan Younis huko Gaza iliharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya IsraelPicha: AFP/Getty Images

Jeshi la Israel limesema Ahmed Abdullah Abu Shalal alikuwa amehusika na mashambulio kadhaa ya kigaidi katika mwaka uliopita, ikiwa ni pamoja na shambulio kwenye eneo la Jerusalem mashariki. Abu Shahal aliuwawa kufuatia shambulio la anga dhidi ya gari alilokuwemo, ilielezea taarifa ya jeshi iliounganishwa na video inayoonesha shambulio hilo.

Wizara ya afya ya Palestina huko Ramallah ilisema mwili wa shahidi asiyejulikana aliyeuawa na uvamizi  wa Israel kwa kulipuliwa gari umepokelewa na hospitali huko Nablus.

''Tumechukua hatua madhubuti''

Msaada wa kibinadamu zikiwemo dawa na mahitaji mengine ya kimsingi kwa mateka wa Israel na raia wa Palestina unatarajiwa kuwasili katika ukanda wa Gaza kuanzia leo chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Qatar na Ufaransa, siku moja tu baada ya mashambulizi mabaya ya anga upande wa kusini mwa Gaza. Rais wa Ufaransa Emmaneul Macron amesema kipaumbele huko Gaza ni usitishwaji mapigano.

 ''Tumechukua hatua madhubuti. Na lazima niseme, ilikuwa haijawahi kutokea kwa nchi ya Magharibi tangu mwanzo. Kwanza, kwa kupeleka rasilimali za kijeshi, hasa hospitali ya Dixmude, ambayo itakaa hadi mwisho wa mwezi na ambayo tayari imeweza kutibu zaidi ya wagonjwa 1,000, watoto na watu wazima.''

Idadi ya vifo yaongezeka Gaza

Msaada wa kibinadamu kuwasilishwa kwa mateka na raia wa Palestina ukanda wa GazaPicha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema leo kuwa idadi ya vifo kufuatia vita baina ya Israel na Hamas huko Gaza inafikia zaidi ya elfu 24 toka Oktoba Saba. Taarifa ya wizara ilisema watu wengine 61,504 pia wamejeruhiwa katika ardhi ya Palestina wakati wa vita.

Wakati huohuo, Iran imefanya mashambulizi kwenye ardhi ya Pakistan ikizolenga kile imesema kuwa ngome za kundi la wanamgambo wa Jaish al Adl, ikiwa ni siku moja tangu ilipoyashambulia maeneo kadhaa nfdani ya Syria na Irak. Pakistan imearifu kuwa mashambulizi hayo ya Iran yamewauwa watoto wawili na kujeruhi watu wengine watatu.

Mito ya utulivu Mashariki ya Kati

Pakistan imelaani mashambulizi hayo kwa matamshi makali ikisema ni uingiliaji wa makusudi wa anga yake. Mashambulizi hayo yanatishia kuzusha mvutano kati ya nchi hizo mbili ambazo zina mahusiano ya kidiploamasia lakini mara zote hutizamana kwa jicho la tahadhari.

China imezitolea mwito Pakistan na Iran wa kujizuia. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Mao Ning amesema nchi yake imezitaka Iran na Pakistan kuepuka vitendo ambavyo vinaweza kusababisha kuongezeka kwa mvutano kati yao. Kiongozi wa kanisa katoliki Dunia, Papa Francis pia alilaani vikali shambulio la Iran huko Irak na kutoa mwito wa pande zote kujizuia.

 

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW