1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kuishambulia Gaza, 7 wauwawa

Amina Abubakar dpa/reuters
6 Oktoba 2025

Watu 7 wameripotiwa kuuwawa katika shambulizi la Israel Ukanda wa Gaza huku majadiliano yakiendelea Misri ya namna ya kuutekeleza mpango wa amani wa rais wa Marekani Donald Trump wa usitishaji vita katika Ukanda huo.

Mgogoro wa Mashariki ya Kati
Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza licha ya juhudi za kusitisha vita kuendelezwa MisriPicha: Mohammed Skaik/TheNews2/IMAGO

Shirika la habari la Palestina WAFA limesema watu wawili wameuwawa karibu na taasisi ya kugawa chakula inayoendeshwa na shirika la misaada linaloungwa mkono na Marekani na Israel la Gaza Humanitarian Foundation, GHF. 

WAFA imedai wanajeshi wa Israel waliwamiminia risasi wapalestina, waliokuwa wanasubiri msaada huo wa kiutu. Hata hivyo masemaji wa jeshi la  Israel amesema jeshi lake halina taarifa hiyo, huku GHF ikisema hakuna tukio lolote lililoripotiwa na operesheni ya kugawa chakula inaendelea vizuri. Taarifa kutoka pande zote mbili hazikuweza kuthibitishwa mara moja. 

Haya yanajiri wakati mazungumzo ya wajumbe wa Hamas na Israel, yakiendelea nchini Misri ya kujadili mpango wa amani ya Gaza uliopendekezwa na rais wa Marekani Donald Trump. 

Israel yasema kamwe haiwezi kuitambua Palestina kama dola huru

Lengo la mpango huo ni kuwaachia mateka wote 48 walio hai na waliokufa wanaoshikiliwa na Hamas ili nalo kundi hilo liwapokee wafungwa wa kipalestina walioko vizuizini nchini Israel. Masuala mengine katika mpango huo kama kuwapokonya silaha kundi la Hamas, na Israel kuwaondoa kikamilifu wanajeshi wake Gaza ni mambo ambayo bado yanaleta mvutano mkubwa. 

Hamas imesema haitoweka silaha zake chini hadi pale Israel itakapowaondoa wanajeshi wake Gaza na kuitambua Palestina kama dola huru huku Israel nayo ikisema hilo halitowezekana. 

Trump aitaka Israel kusitisha mashambulizi yake Gaza

Kwengineko rais Donald Trump aliitolea mwito Israel kuacha kuishambulia Gaza haraka iwezekanavyo ili kutoa nafasi ya mateka kuachiwa na kupitishwa kwa salama. Israel imejibu ikisema itapunguza na sio kusitisha mashambulizi yake hadi pale makubaliano kamili yatakapofikiwa. 

Rais Donald Trump aitaka Israel kuacha kuishambulia Gaza haraka iwezekanavyo ili kutoa nafasi ya mateka kuachiwa na kupitishwa kwa salama.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Huku hayo yakiarifiwa Iran imesema inaunga mkono juhudi zozote, zitakazositisha mgogoro unaoendelea sasa Gaza. Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Jamhuri hiyo ya kiislamu Esmail Baghaei, amesema juhudi za kusitisha mauaji ya halaiki Gaza yanaungwa mkono. 

"Tunakaribisha hatua yoyote wakati huu itakayopelekea kusitishwa kwa mauaji ya halaiki  Gaza, na kufanya hali kuwa tulivu ili kuwezesha misaada kufikishwa kwa watu wanaokandamizwa wa Palestina inayokaliwa kimabavu."

Baghaei bila ya kutoa ufafanuzi alisema Iran ina wasiwasi mkubwa wa mpango wa amani ya Gaza uliopendekezwa na Trump. Iran ni mshirika mkubwa wa wanamgambo wa kipalestina wa Hamas. 

Wakati huo huo kundi la uhamasishaji la Israel linalotetea kuachiwa kwa mateka wa Israel nchini Gaza, limemtaka Rais Trump kupewa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kuleta amani katika kanda ya Mashariki ya Kati. 

Katika barua iliyotumwa kwa kamati ya Nobel ya Norway kundi hilo limesema Trump tayari amewezehsa kile wengi walichosema hakiwezekani. Kundi hilo limesemaTrump amesema hatofumba jicho hadi mateka wote watakapoachiwa Gaza na hilo pekee linapswa kumpitisha Trump kama mtu sahihi anayestahili kutunukiwa tuzo hiyo. 

Trump amekuwa akisema hadharani kwamba anastahili kupewa tuzo hiyo ya amani ya Nobel, japo wataalamu wanasema nafasi yake ni ndogo mno. 


 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW