1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza

16 Septemba 2024

Maafisa wa Palestina wamesema makombora yaliyovurumishwa na Israel katika Ukanda wa Gaza, yamesababisha vifo vya watu 16 wakiwemo wanawake watano na watoto wanne. Vita vya Gaza vinakaribia mwaka mmoja.

Gaza| Mashariki ya Kati
Wizara ya afya ya Gaza imesema wapalestina zaidi ya 41,000 wameuwawa tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas mnamo Oktoba 7Picha: Moez Salhi/Anadolu/picture alliance

Kombora lililorushwa upande wa Gaza liliharibu nyumba moja katika eneo lililojaa watu katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa mji huo na kuwauwa watu 10 ikiwa ni pamoja na wanawake wanne na watoto wawili. Hopsitali ya Awda iliyopokea miili ya watu hao ilithibitisha idadi hiyo na pia kuthibitisha kujeruhiwa kwa watu wengine 13. Rekodi za hospitali zinaonesha waliouwawa ni mama, mtoto wake na ndugu zake watano.

Shambulizi jengine lililolenga pia nyumba moja mjini Gaza lilisababisha vifo vya watu 6 akiwemo pia mwanamke na watoto wake wawili. Hata hivyo Israel imesema imekuwa ikiwalenga wanamgambo na kulishutumu kundi la Hamas na makundi mengine yaliyojihami kuhatarisha maisha ya raia kwa kuendesha operesheni zao katika maeneo ya makaazi ya watu.

Marekani kuishinikiza Israel kutoshambulia maeneo ya kiutu

Kwengineko kundi la Hamas limedai lina rasilimali za kutosha kuendelea na vita hivyo vinavyokaribia mwaka mmoja. Afisa mmoja mkuu wa kundi la Hamas Osama Hamdan ameliambia shirika la habari la AFP kwamba bado wataendelea kupambana vikali katika vita hivyo. Kauli yake ameitoa wiki moja baada ya waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant kusema wameshalitokomeza kundi la kijeshi la Hamas.

Gallant asema matumaini ya kusitisha mvutano kati ya Israel na Hebollah yanafifia

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant Picha: Michael Reynolds/EPA

Shambulizi la leo linafanyika wakati waziri wa Ulinzi wa Israel akionya juu ya kufifia matumaini ya kusitisha vita vyake na makundi ya wanamgambo wa Hezbolla mpakani mwa Lebanon na hivyo kuanzisha tena hofu ya kutanuka kwa vita katika kanda nzima. Gallant amemwambia mwenzake wa Marekani Lloyd Austin kwamba vita kati ya pande hizo mbili havitakwisha, kwasababu bado Hezbollah inaendelea kujifungamanisha na kundi la Hamas.

Kundi hilo limekuwa likitekeleza mashambulizi dhidi ya vikosi vya Israel kupinga Israel kuendelea kuishambulia Gaza. Amos Hochstein, mjumbe maalum wa rais wa Marekani Joe Biden amewasili Israel kusaidia kutuliza mvutano kati ya Israel na Hezbollah.

Israel yafanya mashambulizi Palestina, Syria na Lebanon

Huku hayo yakiarifiwa wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na kundi hilo la Hamas imesema wapalestina zaidi ya 41,000 wameuwawa tangu Israel ilipoanza kuishambulia Gaza mnamo Oktoba 7 na kuchochoea vita vya pande hizo mbili vinavyoendelea kwa sasa katika kanda ya Mashariki ya kati.

Wizara hiyo haitofautishi vifo vya raia na vile vya wanamgambo lakini imesema nusu ya idadi ya waliouwawa ni wanawake na watoto. Israel kwa upande wake imesema imeshawaangamiza hadi sasa wanamgambo 17,000 bila ya kutoa ushahidi.  vIta hivyo vimesababisha uharibifu mkubwa wa Mali na kuwakosesha makaazi asilimia 90 ya idadi jumla ya watu wa Gaza milioni 2.3.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

01:35

This browser does not support the video element.

Vyanzo: ap/afp

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW