1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza operesheni Ukingo wa Magharibi

30 Agosti 2024

Vikosi vya Israel vimemuua kamanda wa Hamas katika mji wa Jenin Ijumaa wakati vikiendeleza operesheni kubwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu kwa siku ya tatu, na kufikisha vifo 19 kutokana na kampeni hiyo.

Ukingo wa Magharibi | Operesheni ya Israel Ukingo wa Magharibi
Jeshi la Israel limeitaja operesheni yake kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi kuwa ya kupambana na ugaidi.Picha: Mohammed Turabi/IMAGESLIVE/ZUMA Press Wire/picture alliance

Israel imefanya shambulio la angani katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa leo Ijumaa wakati operesheni yake kubwa ya kijeshi ikiingia siku ya tatu, huku pande zote mbili zikiripot kuwa Wapalestina wasiopungua 16 wameuawa.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa operesheni hiyo iliyoanzishwa siku ya Jumatano, inachochea hali ambayo tayari ni tete na kuitaka Israel kuikomesha mara moja.

Wakati huo huo, afisa wa juu wa misaada wa Umoja wa Mataifa amehoji "kilichousibu ubinadamu", mnamo wakati vitia vikiendelea Gaza na operesheni za kiutu zikikumbana na vikwazo lukuki.

Israel imeutaja uvamizi wake wa miji na kambi za wakimbizi kote kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi kuwa ni operesheni ya kupambana na ugaidi ambapo kufikia sasa Wapaestina wasiopungua 16 wameuawa, idadi hii ikithibitishwa pia na wizara ya afya ya Palestina.

Jeshi la Israel limesema moja ya "ndege zake ilishambulia kikundi cha ugaidi" karibu na mji wa Jenin mapema Ijumaa, bila hata hivyo kutoka ufafanuzi.  Mwandishi wa shirika la habari la AFP ameripoti milipuko mikubwa kutoka kambi ya wakimbizi mjini humo, na moshi mkubwa ukitanda haraka kutokea eneo hilo.

Vikosi vya Israel vikiwa kwenye mtaa ulio karibu na kambi ya wakimbizi ya Nour Shams, mjini Tulkarem, Agosti 29,2024.Picha: Nidal Eshtayeh/Xinhua/IMAGO

Jeshi la Israel limesema pia kuwa polisi wa mpakani wamemuuwa Wassem Hazem, aliekuwa kiongozi wa Hamas mjini Jenin, na anaedaiwa kushiriki mashambulizi ya mabomu katika eneo hilo la Wapalestina.

Vikosi vya Israel viliondoka kwenye miji mingine ya Ukingo wa Magharibi Alhamisi jioni, lakini mapigano yameendelea karibu na Jenin, ambao kwa muda mrefu ni kitovu cha shughuli za wapiganaji.

Israel yakubali kupisha kampeni ya chanjo ya polio

Katika Ukanda wa Gaza, makombora ya Israel yamepiga maeneo ya magharibi mwa mji wa Gaza mapema Ijumaa, huku duru za kitabibu katika hospitali ya kusini ya Nasser zikisema shambulio la israel limeuwa watu watatu mjini Khan Younis.

Soma pia: Israel kusitisha mapigano Gaza kwa siku 3 kupisha chanjo ya Polio

Shirika la afya duniani, WHO, limesema israel ilikubali usimamishaji wa mapigano wa kiutu kwa angalau siku tatu katika baadhi ya maeneo ya Gaza kuanzia Jumapili, ili kuwezesha utoaji wa chanjo, baada ya kisa cha kwanza cha polio kurikodiwa katika eneo hilo baada ya takribani miaka 25.

Hata hivyo waziri mkuu wa Israel Bin Yamin Netanyahu alisema hatua hizo siyo "usitishaji vita."

Karibu dozi milioni 1.2 za chanjo ya polio zimewasili Gaza kuelekea kuanza kwa kampeni hiyo ya chanjo Septemba 1, ambayo inawalenga watoto 640,000, amesema afisa wa WHO siku ya Ijumaa.

Takribani dozi 400,000 za ziada ziko njiani kupelekwa eneo hilo, alisema Rik Peeperkorn, mwakilishi wa WHO katika maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

01:35

This browser does not support the video element.

Kamala Harris asisitiza haja ya kumaliza vita

Nchini Marekani, Makamu wa Rais Kamala Harrsi ameahidi kuwa hatobadili sera ya Washington ya kuipatia silaha Israel ikiwa atachaguliwa kuwa rais mwezi Novemba, lakini amesisitiza wakati umefika kukomesha vita hivyo.

Akizungumza katika mahojiano yake ya kwanza ya televisheni tangu kuteuliwa na chama cha Democratic kuwa mgombea wake wa urais, Harris, amekariri dhamira ya kuhakikisha usalama wa Israel na haki yao ya kujilinda tangu shambulio la Oktoba 7.

Lakini Makamu huyo wa Rais ameongeza kuwa namna Israel inavyoendesha vita vyake dhidi ya Hamas pia ni muhimu, akigusia vifo vilivyozidi vya raia wa Gaza kutokana na vita hivyo, na kusisitiza haja ya kufikia mapatano ya kusitisha vita hivyo.

Soma pia: DNC: Kamala Harris aihimiza Marekani kuchukua mwelekeo mpya

''Makubaliano sio tu jambo sahihi la kufanya ili kumaliza vita hivi, lakini yatatoa mwelekeo wa mengi yanayopaswa kutokea baadaye. Naendelea kujitolea tangu Oktoba 8, kwa kile tunachopaswa kufanya ili kufanikisha suluhisho la mataifa mawili, ambapo Israel iko salama na kwa kiwango sawa, Wapalestina wana usalama na kujiamulia mambo yao na heshima,'' alisema Harris katika mahojiano na kituo cha CNN.

Shambulio la Hamas la Oktoba 7 lilisababisha vifo vya watu 1,199, wengi wao raia kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Israel, huku wapiganaji pia wakiwachukuwa mateka watu 251, ambapo 103 kati yao wanaendelea kushikiliwa Gaza, wakiwemo 33 ambao jeshi la Israel linasema wamekufa.

Kampeni ya kisasi ya Israel imesababisha vifo vya watu wasiopungua 40,602 Gaza, na Umoja wa Mataifa unasema wengi wao ni wanawake na watoto. Vita hivyo vimeuharibu kabisaa Ukanda wa Gaza, kuwahamisha mara kwa mara wakazi wake milioni 2.4, na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.