1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya mashambulizi ya kuwalenga Hamas Gaza

10 Julai 2024

Vikosi vya Israel vimefanya mashambulizi makubwa zaidi kote katika Ukanda wa Gaza leo, ambayo yamewalenga wapiganaji wa Hamas wanaoendesha shughuli zao ndani ya jengo la umoja wa Mataifa.

Ukanda wa Gaza | Wanajeshi wa Israel
Wanajeshi wa Israel wakiwa katika eneo la GazaPicha: Leo Correa/dpa/AP/picture alliance

Jeshi la Israel pia limesema linachunguza shambulio la jana ambalo duru za hospitali zilisema watu wasiopungua 29 waliuawa katika shule mjini Khan Younis, la nne kulenga majengo ya shule katika muda wa siku nne.

Mapema leo Jumatano, watu wanne wameuawa na mmoja kujeruhiwa vibaya katika shambulio la bomu lililolenga nyumba katikati mwa mji wa Nuseirat, na watu wengine wawili waliuawa na sita kujeruhiwa katika shambulio lingine dhidi ya nyumba eneo la Bani Suhaila, karibu na Khan Yunis, kulingana na vyanzo vya hospitali.

Israel imeongeza mashambulizi ya anga na ardhini katika mji wa Gaza na kusini mwa Gaza tangu ilipotoa amri ya kuhama kwa makumi ya maelfu ya watu katika eneo eneo la Wapalestina lililoharibiwa vibaya na vita. 

Soma pia:   Jeshi la Israel laushambulia vikali Ukanda wa Gaza

Ongezeko la mashambulizi hayo ya kijeshi linakuja wakati maafisa wa Israel wakianza mazungumzo nchini Qatar leo, yanayolenga kufikia muafaka katika vita vinavyoendelea tangu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7.

Jeshi la Israel limesema shambulio moja la usiku katika mji wa Gaza lililenga shabaha za wapiganaji wa Hamas na Islamic Jihad wanaofanyia kazi ndani ya makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa halijakuwa na udhibiti wa jengo hilo tangu Oktoba. Vikosi vya Israel vilisema mwezi Februari kuwa vimegundua handaki la Hamas chini ya makao makuu hayo.

UNRWA haikuwa na maoni ya mara moja kuhusu shambulio hilo, lakini imesema haina njia ya kuthibitisha madai kwamba vituo vyake vinatumiwa na Hamas na washirika wake.

Shambulio la shule lazusha shutuma kwa Israel

Shambulio baya la Jumanne karibu na shule ya Al-Awda iliyoko Abasan, karibu na Khan Yunis, limesababisha shtuma kali kutoka kwa Hamas kuhusiana na mbinu za kijeshi za Israel.

Picha: EYAD BABA/AFP via Getty Images

Serikali ya Hamas ilisema wengi wa waathirika wa shambulio hilo walikuwa wanawake na watoto. Moja wa mashuhuda wa shambulio hilo, Ghazal Nasser, anasema shambulio hilo ni kama la kustukiza.

"Kulikuwepo na majeruhi na mashahidi. Nilishuhudia hili..watu walitupwa huku na kule na vipande vya miili vilitapakaa, damu." Alisema Nasser.

Soma pia:Wapalestina waendelea kuyakimbia mashambulizi ya Israel Gaza   

Jeshi la Israel lilisema linachunguza ripoti kuhusu mauaji ya raia karibu na shule ya Al Awda, ambayo ilikiri kuwa "karibu na eneo la shambulio. 

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema leo kuwa asilimia 60 ya wapiganaji wa Hamas wameuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi ya Gaza, inagwa ripoti ya uchunguzi wa gazeti la New York Time ilibainisha kuwa asilimia 70 ya wapiganaji hao hawajaguswa na mashambulizi hayo.

Akizungumza katika bunge la Israel, waziri Gallant pia amesema Israel imevunja sehemu kubwa ya bataliani 24 ambazo tawi la kijeshi la Hamas lilikuwa nazo mwanzoni mwa vita. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW