1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya mashambulizi ya anga Gaza

20 Februari 2024

Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi ya anga huko Gaza na kuwaua wapiganaji kadhaa wa kundi la Hamas na kuharibu maghala ya silaha katika kitongoji cha Khan Younis.

Gaza|
Vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 28,000 wakiwemo wanawake na watotoPicha: MOHAMMED SALEM/REUTERS

Katika taarifa ya pamoja, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, na Shirika la Afya Duniani yamesema magonjwa, ukosefu wa chakula na maji safi, vinaweza kusababisha ongezeko la vifo vya watoto huko Gaza.

"Wakati mashambulizi ya mabomu yakiendelea Gaza, wasiwasi wa afya ya umma unaongezeka huku wanawake wakiathirika zaidi. Shirika la Umoja wa Mataifa la wakazi linaonya kwamba kila mtu huko Gaza anakabiliwa na njaa, ikiwa ni pamoja na wanawake wajawazito 50,000. Sisi na washirika wetu tunafanya kila tuwezalo ili kutoa msaada wa chakula katika Ukanda wa Gaza licha ya changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga na mapigano makali," alisema msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujjaric.

Umoja wa Mataifa: Hali Ukanda wa Gaza inatisha

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaipigia kura rasimu iliyopendekezwa na Marekani ya kutaka usitishwaji wa muda wa mapigano na kupinga mashambulizi ya jeshi la Israel katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah.