1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yafanya mashambulizi ya anga Gaza

24 Aprili 2024

Vikosi vya Israel vimefanya mashambulizi ya anga huko Gaza katika vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Hamas.

Miundombinu ya Khan Younis ikiwa imeharibiwa kwa vita
Miundombinu ya Khan Younis ikiwa imeharibiwa kwa vitaPicha: AFP

Mapema Jumatano asubuhi duru za hospitali na usalama zimeripoti kuhusu mashambulizi ya anga ya Israel huko Rafah, pamoja na kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.

Mwandishi wa shirika la habari la Ufaransa, AFP na watu walioshuhudia wameripoti pia kuhusu miripuko mikubwa kwenye maeneo kadhaa ya kaskazini mwa Gaza wakati wa usiku, huku jeshi la Israel likisema kuwa ndege yake ya kivita imeshambulia zaidi ya maeneo 50 waliyoyalenga katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Wapalestina wayakimbia makaazi yao

Baadhi ya raia wa Kipalestina walionekana wakiyakimbia makaazi yao kaskazini mwa Gaza Jumatano, wiki chache tu baada ya kurejea, kwa sababu ya mashambulizi ya Israel ambayo wamesema yalikuwa mabaya sawa na yale ya mwanzo wa vita.

Mashambulizi mengi yalielekezwa huko Beit Lahiya, kaskazini mwa Gaza, ambako jeshi la Israel limetoa amri ya kuondolewa kwa watu kwenye vitongoji vinne hapo jana Jumanne, likionya kuwa wako kwenye eneo hatari la mapigano.

Kambi wanayoishi Wapalestina walioyakimbia makaazi yao GazaPicha: Bassam Masoud/REUTERS

Wakati huo huo, Gian Carlo Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, amesema wakaazi wa Gaza wanaweza kukabiliwa na baa la njaa ndani ya wiki sita zijazo, kutokana na kuongeza kwa hatari ya njaa kila siku.

''Tunakadiria kuwa asilimia 30 ya watoto, wenye chini ya umri wa miaka miwili kwa sasa wana utapiamlo, na asilimia 70 ya wakazi wa kaskazini mashariki wanakabiliwa na njaa mbaya. Kuna ushahidi wa kuridhisha kwamba njaa, uhaba wa chakula, utapiamlo na vifo vitashuhudiwa katika wiki sita zijazo,'' alibainisha Carlo.

WFP: Chakula kisambazwe Gaza kila siku

Akizungumza Jumatano mjini Geneva, Uswisi, Carlo amesema njia pekee ya kuepusha njaa huko Gaza ni kuhakikisha usambazaji wa chakula unafanyika mara moja na kila siku.

Ama kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu taarifa za kugundulika makaburi ya pamoja katika hospitali mbili za Gaza ambazo ziliharibiwa wakati Israel inalizingira eneo hilo, na majibu ya kina yatolewe.

Picha: Xavier Lejeune/European Union, 2020

Msemaji wa umoja huo Peter Stano amesema hilo ni jambo ambalo linawalazimisha kutoa wito wa uchunguzi huru wa tuhuma zote na kwa kuzingatia mazingira yote, kwa sababu kwa hakika inajenga hisia kwamba inawezekana kuna ukiukwaji wa haki za binadamu.

Israel imekanusha madai hayo yaliyotolewa na Palestina na kusema kuwa hayana msingi wowote.

Soma zaidi: Israel yakanusha madai kuhusu makaburi ya pamoja Gaza

Naye Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, amesema Jumatano kuwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel yamewaua nusu ya makamanda wa Hezbollah kusini mwa Lebanon, wakati wa mapigano ya mpakani ambayo yalipamba moto sambamba na vita vya Gaza tangu mwezi Oktoba.

(DPA, AFP, AP, Reuters)