Israel yafanya mashambulizi ya angani Ukanda wa Gaza
5 Julai 2023Israel imefanya mashambulizi ya angani katika Ukanda wa Gaza kujibu makombora yaliyorushwa kutokea eneo hilo la huo la pwani la Kipalestina. Jeshi la Israel limesema limeyafanya mashambulizi hayo usiku wa kuamkia leo baada ya makombora matano kufyatuliwa kutokea Gaza. Jeshi limesema makombora hayo yaliharibiwa na mfumo wake wa ulinzi wa angani wa Iron Dome. Chanzo cha usalama cha Palestina kimesema mashambulizi ya Israel yalililenga eneo la kijeshi la Hamas kaskazini mwa Gaza lakini hayakusababisha majeruhi. Hayo yamefanyika wakati jeshi la Israel lilianza kuwaondoa askari wake kutoka Jenin, katika Ukingo unaokaliwa wa Magharibi baada ya operesheni kuu ya siku mbili katika eneo hilo. Wapalestina 12 na mwanajeshi mmoja wa Israel waliuawa wakati wa operesheni hiyo kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin, iliyoanzishwa mapema Jumatatu chini ya serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.