1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hadar Goldin, aliyetekwa na Hamas azikwa Israel

Amina Abubakar ap/afp/reuters
11 Novemba 2025

Maelfu ya waisraeli wameshiriki maziko ya mwanajeshi Hadar Goldin ambae mwili wake ulirejeshwa nyumbani zaidi ya miaka 11, baada ya kutekwa na Hamas.

Israel Tel Aviv 2025 | Hadar Goldin
Israel yafanya mazishi ya mwanajeshi aliyerudishwa na Hamas baada ya miaka 11Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Mamaake Goldin, Lea Goldin, alionekana akibubujikwa na machozi huku akiiambia maiti ya mwanawe kwamba " Kwa miaka 11 tumekusubiri. Nakupenda sana Hadar, pumzika kwa amani."

Wazazi wa mwanajeshi huyo wamekuwa wakiishutumu serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa kwa miaka 11 imemtelekeza mpendwa wao Hadar Goldin, aliyetekwa na kuawa na wanamgambo wa Hamas mnamo Agosti mosi mwaka 2014, muda mfupi baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka huo kati ya Israel na Hamas.

Mwili wake ndio uliokuwa unashikiliwa pekee na wanamgambo hao kabla ya kutokea mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel yaliyochcoea mzozo unaoshuhudiwa sasa Mashariki ya Kati.

Bunge la Israel limepitisha muswada ambao utatoa adhabu ya kifo kwa wanamgambo wa Palestina watakaoshitakiwa kwa mauaji ya raia wa Israel.Picha: GIL COHEN-MAGEN/AFP/Getty Images

Hamas iliurejesha mwili huo kama sehemu ya makubaliano mapya ya kusitisha mapigano yaliyofikia Oktoba 10 mwaka huu kati ya pande hizo mbili.

Bunge la Israel lapitisha muswada tete

Huku hayo yakiarifiwa bunge la Israel limepitisha muswada ambao utatoa adhabu ya kifo kwa wanamgambo wa Palestina, watakaoshitakiwa kwa mauaji ya raia wa Israel huku baadhi ya wabunge wakisema hilo litazuwia hatua ya ubadilishanaji wa wafungwa kama inayoonekana kwa sasa. Muswada huo ulipitishwa na wabunge 39 huku 16 wakiupinga kati ya wabunge 120 walioko bungeni.

Awali waziri wa usalama wa taifa la Israel Ben-Gvir, alitoa wito kwa vyama vyote vya kisiasa kuunga mkono muswada huo, akisema unania ya kuutokomeza ugaidi. Muswada huo sasa utasubiri kufikishwa katika kamati ya bunge ili uendelee kujadiliwa zaidi, kabla ya kupigiwa kura tena mara ya pili na mara ya tatu. Hata hivyo haijawa wazi iwapo muswada huo utapita na kuwa sheria kufuatia wabunge muhimu kususia kura ya awamu ya kwanza.

Macron na Abbas kukutana kujadili Gaza

Kwengineko Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kukutana na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmud Abbas mjini Paris kujadili utekelezaji kikamilifu wa makubaliano ya usitishaji wa mapigano mjini Gaza.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kukutana na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmud Abbas mjini Paris kuijadili Gaza.Picha: Christophe Ena/dpa/picture alliance

Katika juhudi  hizo za kuhakikisha makubaliano hayo yanafanikiwa, mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki na Misri pia watakutana kesho Jumatano mjini Ankara, Uturuki kujadili makubaliano ya usitishwaji mapigano Gaza, na juhudi za kimataifa za kuujenga upya ukanda huo baada ya kukumbwa na mashambulizi ya Israel kwa miaka miwili.

Waziri Hakan Fidan wa Uturuki na mwenzake Badr Abdelatty wa Misri watakutana kuzungumzia hatua nyengine ya kuchukua ili kufanikisha makubaliano hayo.

Nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF lPicha: Denis Balibouse/REUTERS

Israel na Hamas wamewkuwa wakinyosheana kidole cha lawama kwa kukiuka makubaliano hayo, Israel ikisema Hamas inajikokota katika mpango wa kurejesha miili ya mateka huku Hamas ikisema Israel inaendelea kuzuwia msaada kuingia Gaza.

UNICEF yasema Israel inazuwia misaada kuingia Gaza

Wakati hayo yakiarifiwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF limesema Israel inazuwia majitaji muhimu kama sindano za kuwachanjia watoto na chupa za maziwa ya watoto kuingia Gaza kuwafikia watu walio na mahitaji.

UNICEF imesema inapata changamoto kubwa kufikisha Gaza, sindano milioni 1.6 na friji zinazotumia umeme wa sola ili kuhifadhi sindano hizo. Sindano hizo zimesubiri kuidhinishwa katika eneo la mpakani kuanzia mwezi Agosti.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW