1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yafanya operesheni kubwa ya kijeshi mjini Jenin

3 Julai 2023

Wapalestina wasiopungua watano wameuawa kutokana na operesheni kubwa ya kijeshi ambayo imefanywa na jeshi la Israel katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi.

Israeli forces strike West Bank city
Picha: Mohamad Torokman/REUTERS

Wizara ya Afya ya Mamlaka ya Wapalestina imesema watu wengine 20 wamejeruhiwa, wakiwemo saba walio katika hali mahututi.

Israel imesema operesheni hiyo iliyopewa jina la siri ‘Nyumbani na Bustanini' ilihusisha mashambulizi toka angani dhidi ya miundo mbinu ya magaidi, na vilevile mashambulizi makali ya ardhini.

Ukumbi mmoja wa sanaa ulioko katikati ya mji huo wa Jenin uliripotiwa kushambuliwa kutoka angani.

Kambi ya wakimbizi ya Jenin iliyo na watu 17,000 pia ililengwa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, jeshi la Israel limesema halitajitia hamnazo wakati lililowaita magaidi wakiendelea kuwajeruhi raia wakitumia kambi ya wakimbizi ya Jenin kama maficho.

Soma pia: Wapalestina wawili wauliwa Ukingo wa Magharibi

Msemaji wa Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas ameitaja operesheni hiyo ya Israel kuwa "uhalifu mpya wa kivita”.

Ameitaka jamii ya kimataifa kuvunja kile alichokiita ‘kimya cha aibu' na ichukue hatua kali.

Kulingana na jarida la Jerusalem Post, shirika la ujasusi wa ndani nchini Israel, Shin Bet, limesema mashambulizi ya angani yalipiga kituo cha kamandi na mawasiliano.

Mashambulizi ya Israel yamelenga miundombinu ya wale iliyowaita kuwa 'magaidi'Picha: Raneen Sawafta/REUTERS

Jarida hilo limeripoti kuwa kituo hicho hutumiwa kama ghala ya silaha, sehemu ya mkutano ya magaidi na vilevile sehemu wanayotumia kufuatilia matukio.

Soma pia: Vikosi vya Israel vyauwa Wapalestina watatu

Kulingana na ripoti hiyo, miundombinu kadhaa pia ilishambuliwa na umeme ulikatika kote mjini Jenin.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amedai jeshi limeendeleza operesheni dhidi ya ngome za ugaidi mjini Jenin. Gallant ameongeza kusema: "Katika kukabiliana na ugaidi, tutachukua hatua kali na yenye maamuzi. Yeyote anayewadhuru raia wa Israel, atalipa gharama kubwa."

Kulingana na madai ya Wapalestina, wanajeshi wa Israel waliingia katika mji wa Jenin muda mfupi tu baada ya mashambulizi ya angani, na wakapambana na wanamgambo wa Palestina.

Mji wa Jenin ulioko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, umekuwa ngome ya kundi la wanamgambo wa Palestina. Mji huo umeshuhudia makabiliano makali ya mara kwa mara kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo hao.

Katika siku za hivi karibuni, hali tete ya usalama kati ya Israel na Wapalestina imezidi kuzorota.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema "yeyote anayewadhuru raia wa Israel, atalipa gharama kubwa."Picha: MENELAOS MYRILLAS/SOOC/AFP via Getty Images

Takriban wiki mbili zilizopita, kulitokea machafuko Ukingo wa Magharibi wakati Wapalestina wawili walipowavamia Waisraeli wanne. Hayo yalifuatiwa na machafuko makubwa yaliyofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo hilo.

Tangu wakati huo, jeshi la Israel limefanya misako mingi katika Ukingo wa Magharibi, hali ambayo imekuwa ikisababisha makabiliano kati ya Wapalestina na wanajeshi wa Israel.

Tangu mwanzo wa mwaka huu, zaidi ya Wapalestina 130 wameuawa na jeshi la Israel. Katika kipindi hicho hicho, Waisraeli 22, mwanamke mmoja wa Ukraine na raia mmoja wa Italia wameuawa kwenye mashambulizi.

Israel ilichukua Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem wakati wa Vita Vya Siku Sita mnamo mwaka 1967.

Wapalestina wanadai maeneo hayo ni jimbo lao na Yerusalemu Mashariki kuwa mji wao mkuu.

Kambi ya Jenin ilikaliwa na wakimbizi wa Kipalestina waliofukuzwa makwao baada ya vita vya 1948 kati ya Israeli na Wapalestina.

(Chanzo: DPAE)