Israel yafanya wimbi jingine la mashambulizi Tehran
1 Machi 2026
Milipuko mikubwa imeripotiwa Jumapili mjini Tehran huku mashambulizi ya Marekani na Israel yakiingia siku ya pili mfululizo. Jeshi la Israel limesema limefanikiwa kuvunja sehemu kubwa ya mifumo ya ulinzi wa anga magharibi na kati mwa Iran, hatua inayodaiwa kufungua "njia kuelekea Tehran.”
Msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Nadav Shoshani, amesema bado kuna malengo mengi yakiwemo viwanda vya uzalishaji wa silaha na miundombinu ya kijeshi. Amesema Israel ina uwezo wa kuendelea na operesheni kwa muda wowote utakaohitajika, lakini kwa sasa hakuna mpango wa kupeleka vikosi vya ardhini nchini Iran. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ametaja kuuawa kwa Khamenei kuwa hatua muhimu ya kimkakati.
"Yeye ndiye aliyeongoza kampeni ya uharibifu dhidi ya Taifa la Israel, aliunda mhimili mzima wa uovu unaotuzunguka, na hata ndani ya Iran aliongoza msimamo mkali usio na maridhiano dhidi ya Taifa la Israel. Kwa hiyo, kuondolewa kwake ni hatua ya mabadiliko makubwa, pamoja na maafisa wengine wengi waandamizi na muhimu walioondolewa pamoja naye.”
Vyombo vya habari vya Iran vimethibitisha kuwa Ayatollah Ali Khamenei, aliyekuwa madarakani tangu 1989, aliuawa akiwa ofisini kwake katika mashambulizi ya Jumamosi. Shambulio hilo pia liliwaua maafisa wa juu akiwemo Mkuu wa Majeshi Abdolrahim Mousavi. Aidha, shirika la habari la ILNA limeripoti kuwa rais wa zamani wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ameuwawa katika shambulio la anga mjini Tehran pamoja na mlinzi wake.
Katika hatua za haraka za kisiasa, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema baraza la uongozi la muda tayari limeanza kazi. Naye Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi, amesema kiongozi mkuu mpya atachaguliwa ndani ya "siku moja au mbili.” Pezeshkian ameahidi kuwa jeshi la Iran "litazivunja kwa nguvu kambi za adui.”
Iran yajibu kwa yashambulizi ya yakombora
Iran imejibu kwa kurusha makombora na droni kuelekea Israel na vituo vya kijeshi vya Marekani katika Ghuba. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi limedai kulenga meli ya kivita ya Marekani, USS Abraham Lincoln, kwa makombora ya balistiki katika eneo la Ghuba. Wakati huo huo, nchini Israel watu sita wameripotiwa kuuawa na zaidi ya 20 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora, huku operesheni za uokoaji zikiendelea.
Kundi la Hezbollah nchini Lebanon limetangaza kuwa liko tayari kukabiliana na Marekani na Israel, ingawa halijathibitisha kuingia rasmi vitani. Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, amesema uamuzi wa vita au amani uko mikononi mwa dola ya Lebanon.
Kimataifa, Rais wa Urusi Vladimir Putin ameyataja mauaji ya Khamenei kuwa ukiukaji wa maadili na sheria za kimataifa. China pia imelaani mashambulizi hayo. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema huu ni wakati wa kihistoria kwa Iran lakini mustakabali wake bado haujulikani.
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa iwapo Iran itaongeza mashambulizi, Marekani itajibu kwa nguvu ambayo "haijawahi kuonekana.”
Athari zimeenea katika ukanda mzima. Nchini Pakistan, watu tisa wameuawa baada ya waandamanaji kuvamia ubalozi mdogo wa Marekani mjini Karachi, huku maandamano pia yakiripotiwa Baghdad karibu na Ukanda wa Kijani.
Athari zakumba ukanda wa Ghuba na dunia
Takriban meli 150 za mafuta na gesi zimeshusha nanga nje ya Mlango wa Hormuz kutokana na hofu ya usalama. Milipuko imeendelea kusikika Dubai na Doha huku mifumo ya ulinzi wa anga ikidungua makombora angani, na kusababisha usumbufu mkubwa wa safari za anga.
Wachambuzi wanasema licha ya pigo kubwa kwa uongozi wa Iran, mfumo wa utawala wa kidini na ushawishi wa Walinzi wa Mapinduzi bado una mizizi imara. Hata hivyo, kasi ya matukio na ongezeko la mashambulizi vinaashiria hatari ya kupanuka kwa vita katika Mashariki ya Kati.