1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafungua tena kivuko cha mpakani cha Kerem Shalom

9 Mei 2024

Israel imesema imekifungua tena kivuko cha mpakani cha Kerem Shalom, kwa ajili ya kuanza tena kuingizwa misaada katika Ukanda Gaza. Vile vile mazungumzo ya kusitisha vita yameanza tena huko nchini Misri.

Israel Kerem Schalom | Außenministerin Baerbock in Israel
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Qatar ambayo ni mpatanishi imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzuia "mauaji ya halaiki" huko Rafah baada ya Israel kukidhibiti kivuko hicho kati ya Gaza na Misri. 

Hatua hiyo ya kufunguliwa kivuko hicho imechukuliwa siku nne baada ya kufungwa mpaka huo ikiwa ni hatua iliyochukuliwa na Israel kujibu mashambulio la roketi yaliyosababisha kuuawa wanajeshi wake wanne.

Jeshi la Israel pamoja na idara inayosimamia maswala ya raia wa Palestina, COGAT, chini ya wizara ya ulinzi ya Israel limesema katika taarifa yake kwamba vya matibabu vilivyotolewa na jumuiya ya kimataifa tayari yamewasili kwenye kivuko hicho.

Kivuko cha mpakani cha Kerem Shalom ni muhimu kwa kupitisha msaada wa kiutu kuingia GazaPicha: Abed Rahim Khatib/dpa

Hata hivyo kivuko muhimu cha Rafah katika Ukanda wa Gaza bado kilikuwa kimefungwa hadi mapema Jumatato baada ya kikosi cha mizinga cha Israel kukiteka na kukidhibiti siku moja iliyopita. Kwa mujibu wa shirika la Habari la Associated Press milio ya hapa na pale ya risasi ilisikilka usiku kucha katika eneo hilo ikijumuisha milipuko miwili mikubwa iliyotokea mapema leo.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema wagonjwa wapatao 46 na watu waliojeruhiwa waliopangiwa kuondoka hapo jana Jumanne kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu nje ya Ukanda wa Gaza wamekwama

Umoja wa Mataifa umesema eneo la kaskazini mwa Gaza tayari limo katika janga la njaa.

Wakati huo huo Qatar ambayo ni mpatanishi katika vita vya Israel na Hamas imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa wa kufanyika kila liwezekanalo kuzuia "mauaji ya halaiki" huko Rafah baada ya majeshi ya Israel kukidhibiti kivuko kati ya Gaza na Misri na imeelezea wasiwasi wake juu ya kitisho cha kutokea mashambulizi makubwa zaidi.

Katika taarifa yake taifa hilo la Ghuba, limehimiza zichukuliwe hatua za haraka za kimataifa ili kuzuia mji huo kuvamiwa hatua itakayosababisha kufanyika uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Kwa upande wake Umoja wa Afrika umelaani hatua ya jeshi la Israel kuingia na kulidhibiti eneo la Rafah kusini mwa Gaza na umeitolea wito jumuiya ya kimataifa kukabiliana na kuongezeka kwa vita. Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, amelaani vikali kurefushwa kwa vita hivi hadi kwenye kivuko cha Rafah.

Kinachoendelea ni kwamba mazungumzo ya kusitisha vita yameanza tena huko nchini Misri na wakati huu pande zote zinazohusika zipo hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya Habari vya mjini Cairo.

Yote hayo yakiendelea Marekani imesitisha zoezi la kupeleka shehena ya mabomu kwenda Israel tangu wiki iliyopita kutokana na wasiwasi kwamba Israel ilikuwa inakaribia kutekeleza maamuzi yake wa kuanzisha mashambulizi ya ardhini kwenye mji wa kusini wa Rafah katika Ukanda wa Gaza.

Israel inaendelea kufanya mashambulizi ya angani katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa GazaPicha: Ramez Habboub/AP Photo/picture alliance

Zaidi ya raia milioni moja wa Palestina wamejihifadhi katika mji wa Rafah baada ya kuhama kutoka kwenye maeneo mengine ya Gaza tangu kuzuka vita vya Israel dhidi ya Hamas, vilivyoanza mara baada ya wanamgambo wa Hamas kuishambulia Israel mnamo Oktoba 7.

Hata hivyo Jeshi la Israel linaonekana kutobabaishwa na hatua ya Marekani ya kusimamisha kupeleka shehena hiyo ya silaha. Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari, ameeleza katika mkutano na waandishi wa Habari kwamba Israel na Marekani ambao ni washirika wa karibu hutatua matatizo yao nyuma ya pazia.

Vita vya Israel dhidi ya Kundi la Hamas vimeingia katika mwezi wa nane sasa tangu vilipoanza.

Vyanzo: AFP/AP/DPA

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

02:51

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW