Israel yaidhinisha mpango wa kuachiwa huru mateka
10 Oktoba 2025
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imetangaza mapema leo Ijumaa kwamba serikali ya Israel imeidhinisha mfumo wa kuachiliwa kwa mateka wote - walio hai na waliofariki". Chapisho fupi kwenye mtandao wa kijamii wa X lililenga kuachiliwa kwa mateka lakini haikutaja sehemu nyingine za mpango wa Rais Donald Trump wa kumalizika vita vya Gaza.
Ofisi hiyo ilisambaza maelezo yaliyotolewa na Netanyahu kwenye mkutano wa kuidhinisha mfumo wa kuachiliwa kwa mateka, pamoja na mjumbe maalumu wa Marekani kwa ajili ya Mashariki ya Kati, Steve Witkoff na mkwe wa Trump Jared Kushner.
Netanyahu alikuwa amekabiliwa na shinikizo kutoka kwa washirika wake wa mrengo mkali wa kulia, huku Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben Gvir akisema atapiga kura kuyapinga makubaliano hayo, akiuita mpango wa kuwaachilia maelfu ya wafungwa wa Kipalestina badala ya mateka 47 waliosalia Gaza "gharama kubwa isiyoweza kuvumilika".
Israel ilisema Alhamisi pande zote zimetia saini awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuwaachilia mateka, na kuongeza kuwa Hamas kuwaachilia mateka "kutakomesha vita hivi".
Makubaliano hayo nchini Misri yanafuatia mpango wa amani wa Gaza wenye vipengele 20 uliotangazwa mwezi uliopita na Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya zaidi ya miaka miwili ya vita vilivyochochewa na shambulio la kundi la Hamas la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.
Trump alisema anapanga kuondoka Jumapili kuelekea Mashariki ya Kati. Misri inapanga hafla ya kusherehekea kukamilika kwa makubaliano hayo, huku rais wa Marekani pia akitarajiwa kupitia nchini Israel na anafikiria kwenda kuiona Gaza iliyoharibiwa.
Timu ya kijeshi ya Marekani kutumwa Mashariki ya Kati
Wakati huo huo, Timu ya kijeshi ya Marekani ya maafisa 200 itatumwa Mashariki ya Kati "kusimamia" usitishaji vita wa Gaza kati ya Israel na Hamas baada ya makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Rais Trump, Jukumu la timu hiyo litakuwa kusimamia, kuchunguza, na kuhakikisha kuwa hakuna ukiukwaji. Maafisa wa kijeshi wa Misri, Qatar, Uturuki na pengine Emarati watajumuishwa kwenye kikosi hicho. Maafisa wa Marekani wamesema "hakuna wanajeshi wa Marekani wanaokusudiwa kuingia Gaza.
Wakati haya yakiarifiwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper amesema Nchi za Ulaya "zote zitakuwa na jukumu lao katika mchakato wa amani wa Gaza. Alikuwa akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje mjini Paris, Ufaransa. Cooper amekabiliwa na maswali kuhusu nafasi ya Ulaya katika utawala wa mpito wa Gaza, baada ya Israel na Hamas kuafikiana kusitisha vita vya miaka miwili.
Cooper amezipongeza Marekani, Qatar, Misri na Uturuki, kwa kuhusika katika mazungumzo yaliyosaidia kufikiwa makubaliano hayo. Alisema jambo la msingi kwa sasa ni kuunga mkono utekelezaji wa awamu ya kwanza lakini pia sote tuwe pamoja kama sehemu ya awamu ya pili.