1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaidhinisha operesheni ya kijeshi Rafah

15 Machi 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameidhinisha operesheni ya kijeshi huko Rafah huku Jeshi la Israel likihakikisha kuwa litawaweka mahali salama raia walioko katika eneo hilo la kusini mwa Ukanda wa Gaza.

 Israel Tel Aviv | Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/AFP/Getty Images

Baada ya Ofisi ya Netanyahu kufahamisha siku ya Ijumaa kuwa operesheni ya kijeshi imeidhinishwa huko Rafah, msemaji wa jeshi la Israel Arye Shalicar amesema kuwa viongozi wa kundi la Hamas pamoja na wapiganaji wengine wa kundi hilo la kigaidi wanashukiwa kujificha katika mji wa Rafah unaopakana na Misri.

Siku ya Alhamisi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisisitiza kuwa Israel itaendeleza  operesheni zake huko Rafah  licha ya shinikizo la kimataifa. Israel inadai kuwa ni vigumu kulitokomeza kundi la Hamas bila kuendesha operesheni huko Rafah.

Lakini jumuiya ya kimataifa inapinga vikali mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika eneo hilo ambalo limekuwa kimbilio la watu karibu milioni 1.5 waliokimbia mapigano katika maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza. Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas imesema idadi ya vifo huko Gaza imefikia watu 31,490.

Watu wakitembea katikati ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa baada ya Israel kushambulia katika mji wa kusini wa Ukanda wa Gaza wa Khan Younis, Machi 13, 2024. Idadi ya vifo vya Wapalestina imeongezeka kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel.Picha: Yasser Qudih/Xinhua/IMAGO

Mapigano makali yameendelea kuripotiwa katika maeneo mengine ya ukanda wa Gaza huku Wapalestina wakishiriki ibada ya funga na sala ya ijumaa katikati ya vifusi na madhila makubwa. Baker Abu Ghiran na Rafaat al-Hameid ni wakaazi wa Gaza:

" Ni Ijumaa ya kwanza ya Ramadhan ya mwaka 2024, vita na mabomu vinaendelea. Tunakusanyika kwenye mabaki ya msikiti wetu ulioharibiwa, tukiswali nje kwenye kivuli. Mwaka huu Ramadhani ni tofauti kabisa kwa sababu ya watu waliuawa, majeruhi, ukosefu wa chakula na ukosefu wa bidhaa muhimu wakati wa Ramadhan. Kuna huzuni, na maumivu lakini Mungu akipenda, tutaendelea kuomba na kufunga licha ya uharibifu na kuzingirwa. Kwa zaidi ya siku 160, tumekuwa katikati ya vifusi hivi, na bado tuko imara."

 

Mashirika ya kiutu yaonya juu ya kitisho cha njaa

Wapalestina wakipokea msaada wa chakula katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan katika Ukanda wa GazaPicha: Mohammed Ali/Xinhua/IMAGO

Mashirika hayo yamesema Wapalestina wanakabiliwa na kitisho cha njaa na yametoa wito wa misaada zaidi kuendelea kuwasilishwa huko Gaza.

Australia imetangaza kurejesha  ufadhili wake kwa shirika la Umoja wa Mataifa  la kutoa misaada kwa Wapalestina (UNRWA), baada ya kusitishwa kutokana na shutuma za Israel kwamba baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo walihusika katika mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Penny Wong, amesema leo Ijumaa kwamba uamuzi huo unalenga kukabiliana na "hali ya kibinadamu huko Gaza ambayo ni mbaya na inazidi kuwa mbaya zaidi." Serikali mjini Canberra inatazamiwa kuipatia UNRWA ufadhili wa dola milioni 3.9 za kimarekani.

Soma pia: Guterres atahadharisha dhidi ya kuishambulia Rafah

Juhudi za kidiplomasia zinaendelea ambapo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anatazamiwa kusafiri kuelekea Jordan na Israel mwishoni mwa juma na anatarajiwa kufanya mazungumzo na Mfalme Abdullah II wa Jordan siku ya Jumamosi na Rais wa Israel Isaac Herzog siku ya Jumapili. Pia, mazungumzo yanayolenga kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano yanatarajiwa kuendelea huko mjini Doha nchini Qatar.

Vyanzo: (afp,ap,rtr,dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW