1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Ulinzi waimarishwa kuelekea maadhimisho ya siku ya Jerusalem

18 Mei 2023

Israel imeimarisha usalama Jerusalem wakati Wayahudi wenye misimamo mikali wanapojiandaa kwa maandamano kwa ajili ya maadhimisho ya kila mwaka ya kumbukumbu ya kutekwa kwa mji huo na vikosi vya Israel mnamo mwaka 1967.

Symbolbild Flagge Israel
Bendera ya IsraelPicha: Jakub Porzycki/NurPhoto/picture alliance

Mapema leo, mamia ya Wayahudi akiwemo Waziri mmoja na wabunge kadhaa kutoka chama cha Likud chake Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na washirika kutoka muungano wake wa kidini na wenye misimamo mikali walifanya ziara katika uwanja wa msikiti wa Al-Aqsa.

Maafisa wa polisi wameshika doria katika maeneo ya karibu ya lango la Damascus, eneo maarufu wanapokutana Wapalestina, na eneo ambalo gwaride la Wayahudi hao litaingia kuelekea mji huo wa kale.

Waandaji wa maandamano hayo wameezeka bendera za Israel katika sehemu mbalimbali za barabarani.

Soma pia:Hali tete Jerusalem kuelekea maandamano ya wafuasi wa itikadi kali Israel 

Maelfu ya Wayahudi wenye misimamo mikali wanatarajiwa kuandamana katika sehemu hasa zinazokaliwa na Waislamu mjini Jerusalem baadae leo, katika hafla ya kila mwaka ambayo inaonekana kuwa ya kichokozi kwa Wapalestina na ambayo pia imezua hofu ya kutokea kwa ghasia.

Ariel Kallner, mbunge na mjumbe wa chama cha Likud anayeshiriki maandamano hayo amesema, "Usalama hauwezi kupatikana kwa kusalimu kwa magaidi, kwa vurugu. Tunahitaji kuwa imara, tunapaswa kuwa imara dhidi ya ghasia, dhidi ya vitisho, na uhusiano wetu na eneo hilo takatifu la Jerusalem ni kitu ambacho hakuna mtu yeyote anayeweza kuukata."

Msikiti wa Al - Aqsa, moja kati ya maeneo takatifu ya Waislamu, uko katika mji mkongwe wa Jerusalem.Picha: Marco Brivio/Zoonar/picture alliance

Maandamano hayo ya kila mwaka, ambayo yanaashiria kutekwa kwa mji wa Jerusalem na vikosi vya Israel mwaka 1967, yanatumika pia kama ishara ya kuonyesha nguvu walizonazo Wayahudi wenye misimamo mikali.

Polisi ya Israel imesema takriban maafisa wa usalama 2,500 wametumwa katika eneo hilo ili kutoa ulinzi na wamejitayarisha kwa lolote lile ikiwemo matukio ya vurugu au hata mashambulizi ya makombora kutoka Gaza.

Soma pia: Israel yaendelea kuwashambulia wanamgambo wa Gaza

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anayeongoza serikali ya kitaifa ya kidini, amesema hafla hiyo litaendelea kama ilivyopangwa.

Msikiti wa Al- Aqsa, moja kati ya maeneo takatifu ya Waislamu, uko katika mji mkongwe huo wa Jerusalem.

Uwanja ulioko msikiti huo pia huchukuliwa kama eneo takatifu kwa Wayahudi, ambao wao hupaita Mlima wa hekalu.

Kwa upande wa Wapalestina, wanatasfiri maandamano ya leo kama sehemu ya kampeni pana ya kuimarisha uwepo wa Wayahudi katika mji huo wa Jerusalem, na wamekasirishwa na hatua ya kuongezeka kwa Wayahudi katika uwanja wa Al-Aqsa, huku baadhi ya Wayahudi wakipuuza marufuku ya kutofanya ibada katika eneo hilo.

Msemaji wa kiongozi wa mamlaka ya Palestine Mahmoud Abbas Nabil Abu Rudeineh, ametahadharisha juu ya kufanyika kwa maandamano hayo aliyoyaita ya kichochezi.

Bwana Rudeineh ameeleza kuwa, kufanyika kwa maandamano hayo kunaashiria wazi kuwa serikali ya Israel imetekwa na Wayahudi wenye misimamo mikali.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW