1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaishambulia Gaza baada ya mpango wa amani kukwama

7 Juni 2024

Kukiwa hakuna ishara ya maendeleo katika juhudi za wapatanishi kufikia usitishaji wa vita Gaza, vikosi vya Israel vimeushambulia mji wa Rafah kutokea angani na ardhini usiku wa Alhamisi, ikilenga tena kambi ya wakimbizi.

Israel | Ndege ya aina ya F-15 ya jeshi la Israel
Israel imeshambulia mji wa Rafah kutokea angani na ardhini baada ya kukwama kwa juhudi za upatanishi.Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Wakaazi wa Rafah wamesema vifaru vya Israel ambavyo vimechukuwa udhibiti kwenye eneo la mpaka na Misri vilifanya mshamnulizi kadhaa kuelekea upande wa magharibi na katikati mwa mji huo, na kujeruhiwa wakaazi wengi waliokuwa wamekwama ndani ya majumba yao na walioshtukizwa na mashambulizi hayo.

Mpalestina mmoja aliezungumza na shirika la habari la Reuters kupitia app ya kuchati, aliutaja usiku wa jana kuwa mmoja ya mbaya zaidi, na kusema vikosi vya ukaliaji vinajaribu kufikia eneo la fukwe la Rafah, akiyaelezea mashambulizi ya jana kuwa ya kimbinu zaidi.

Hata hivyo ameongeza kuwa vikosi hivyo vya Israel vilikabiliwa na mashambulizi makali yaliovilaazimu kurudi nyuma.

Wapalestina wakitembea katika uwanja wa shule inayohifadhi watu waliokosa makaazi ambayo ilishambuliwa na Israel katika eneo la Nuseirat, katikati mwa Gaza.Picha: Bashar Taleb/AFP/Getty Images

Wahudumu wa afya wameripoti pia kuwa vikosi vya Israel vimefanya operesheni ndani ya kambi ya wakimbizi ya Al-Bureij iliyoko katikati mwa Ukanda wa Gaza, huku vikiendelea kuzishambulia kwa ndege na vifaru kambi nyingine mbili na mji wa karibu, na kuuwa na kujeruhi Wapalestina kadhaa.

Soma pia: Hamas, Fatah kufanya mazungumzo ya maridhiano China

Matawi ya kijeshi ya makundi ya Hamas, Islamic Jihad na makundi mengine madogo yameripoti kuwa wapiganaji wao wamefanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya uvamizi vya Israel katika maeneo kadhaa katikati na kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Wapatanishi kutoka Qatar na Misri, wakiungwa mkono na Marekani, wamezidisha juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha vita, kukomesha uhasama na kuwachiwa kwa mateka wa Israel na Wapalestina walioko kwenye magereza ya Israel, lakini vyanzo vya karibu na mazungumzo hayo vimesema hakujawa na dalili ya mafanikio.

Wapatanishi wasubiri jibu la Hamas

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed al-Ansari alisema jana jioni kwamba mpaka sasa kundi la Hamas halijatoa jibu kuhusu pendekezo la usitishaji vita lililowasilishwa na Marekani, na kuongeza kuwa kundi hilo limefahamisha kwamba bado linaendelea kupitia pendekezo hilo.

Afisa wa juu wa Hamas Osama Hamdan ameishtumu Israel kwa kutaka kuendeleza vita Gaza.Picha: Hassan Ammar/AP/picture alliance

Hata hivyo afisa wa juu wa Hamas Osama Hamdan, ameitupia lawama Israel kwa kutaka kuendeleza vita.

"Bila msimamo wa wazi kutoka Israel kukubali usitishaji vita wa kudumu na kujiondoa kikamilifu kutoka Gaza, hatuwezi kukubali mpango usiohakikisha, kuthibitisha, au kudhamini usitishaji vita wa kudumu na kuondoka kikamilifu kutoka Gaza," alisema Osama.

Soma pia: Qatar yataka misimamo ya wazi kuhusu mpango wa Gaza

Vita vya Gaza vilivyosababishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7 mwaka jana, ambapo watu karibu 1,200 waliripotiwa kuuawa, vimeua Wapalestina wasiopungua 36,654 kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.

Uhispania yazidi kuitunisia misuli Israel

Israel imekabiliwa na kutengwa kimataifa kutokana na idadi kubwa ya raia waliouwa katika mashambulizi yake, wengi wao wakiwa watoto, kukiwa na kesi kadhaa katika mahakama za kimataifa zikiishtumu kwa uhalifu wa kivita na mataifa kadhaa ya Ulaya yakichukuwa hatua kulitambua taifa la Palestina.

Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Jose Manuel Albares akifanya mkutano wa habari kwenye makao makuu ya wizara yake mjini Madrid, Juni 6, 2024, ambapo alitangaza azma ya Uhispania kujiunga na kesi ya Afrika Kusini katika ICJ, dhidi ya Israel.Picha: AFP via Getty Images

Uhispania, ambayo ilisababisha ghadhabu nchini Israel wiki iliyopita kwa kulitambua rasmi taifa la Palestina, ilisema Alhamisi kuwa itakuwa nchi ya karibuni zaidi kujiunga kwenye kesi ya Afrika Kusini katika mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, ikiituhumu Israel kwa mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Palestina.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amekubali mwaliko wa wabunge wa Marekani kuihutubia Congress katika kikao cha pamoja cha mabaraza ya Wawakilishi wa Seneti hapo Julai 24 kulingana na duru kutoka Congress.