Israel yaishambulia tena Beirut
1 Aprili 2026
Jeshi hilo limedai kuwa mashambulizi hayo yalimlenga kamanda wa ngazi za juu wa kundi la Hizbullah na yule liliyomuita "gaidi mwengine mkubwa".
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka Wizara ya Afya ya Lebanon, watu saba waliuawa kwenye mashambulizi hayo na wengine 21 walijeruhiwa.
Wakaazi wa huko wameripoti miripuko mikubwa na moto karibu na uwanja wa ndege wa Beirut.
Awali, wanamgambo wa Hizbullah walikuwa wamerusha makombora na droni kuelekea kaskazini mwa Israel, ambako watu kadhaa wanatajwa kujeruhiwa.
Israel, iliyoivamia tena Lebanon baada ya Hizbullah kujiunga na vita vinavyoendelea dhidi ya Iran, imesema inapanga kulitwaa na kulikalia eneo la kusini mwa Mto Litani, lenye ukubwa wa maili 20 kwenye mpaka wake wa kaskazini.
Tayari, Israel imethibitisha kupoteza wanajeshi wake 10, wakiwemo wanne waliouawa jana, kutokana na mashambulizi ya Hizbullah, inayojaribu kuwarejesha nyuma wanajeshi wa Israel.