1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yakanusha madai kuhusu makaburi ya pamoja Gaza

23 Aprili 2024

Jeshi la Israel limekanusha madai ya Palestina kuhusu miili ya Wapalestina kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja na uwezekano wa kufanyika mauaji katika hospitali ya Gaza.

Hospitali ya Al Shifa ikiwa imeharibiwa kwa mashambulizi
Hospitali ya Al Shifa ikiwa imeharibiwa kwa mashambuliziPicha: Tedros Adhanom Ghebreyesus/Handout/REUTERS

Taarifa iliyotolewa Jumanne na jeshi la Israel imeeleza madai kwamba vikosi vya Ulinzi vya Israel, IDF viliizika miili ya Wapalestina hayana msingi wowote na kwmba miili ilifanyiwa uchunguzi katika harakati za kuwatafuta watu waliotekwa na Hamas mwezi Oktoba. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya jeshi, vikosi vyake viliirudisha miili hiyo mahali ilipokuwa imezikwa baada ya kuchunguzwa.

Uchunguzi ulifanyika kwa uangalifu

Jeshi limesema uchunguzi ulifanyika kwa uangalifu na hasa kwenye maeneo ambayo taarifa za ujasusi zilionyesha uwezekano wa kuwapo mateka, na kwamba uchunguzi ulifanyika kwa kuzingatia utu na heshima ya marehemu.

Msemaji wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, amesema kamishna mkuu wa shirika hilo, Volker Turk, ameshtushwa na uharibifu wa kutisha katika vituo vya afya vya Nasser na Al Shifa huko Gaza, na taarifa za kuwepo kwa makaburi ya pamoja ambako mamia ya miili imezikwa.

Hospitali ya Al Shifa, Gaza baada ya jeshi la Israel kuondokaPicha: AFP

''Tumeshtushwa na kusikitishwa pia na uharibifu katika vituo hivyo vya matibabu na kugundulika kwa makaburi ya pamoja ndani na kuzunguka vituo hivyo. Na tunatoa wito wa kufanyika uchunguzi huru, ulio madhubuti na wenye uwazi kuhusu vifo hivyo,'' alifafanua Shamdasani.

Maafisa wa Palestina wiki hii waliripoti kugundulika kwa makaburi ya pamoja katika hospitali ya Khan Younis, baada ya kutelekezwa na majeshi ya Israel. Shamdasani amesema wanaona kuna umuhimu wa kupaza sauti kwa sababu ni wazi miili mingi imegunduliwa. Amesema ofisi yake ilikuwa ikifanya kazi kuthibitisha taarifa za maafisa wa Palestina kwamba miili 283 iligunduliwa Nasser na 30 Al Shifa.

Uongozi wa kisiasa wa Hamas kubakia Doha

Huku hayo yakijiri Qatar imesema uongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas utasalia mjini Doha, ili mradi uwepo wao utaendelea kuwa na manufaa kwa juhudi za upatanishi zinazokusudia kuvimaliza vita huko Gaza.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Qatar, Majed al-Ansari amewaambia leo waandishi habari kwamba Qatar ilifanikiwa kuwa mpatanishi kati ya Israel na Hamas na kufanikisha usitishaji wa mapigano kwa muda wa wiki moja mwezi Novemba, ambapo mateka wengi wa Israel na wa kigeni waliachiliwa huru.

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia wakiwa wanaandamanaPicha: Fatih Aktas/AA/picture alliance

Ama kwa upande mwingine ghasia zilizuka jana kati ya waandamanaji wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina na viongozi wa vyuo vikuu kadhaa vya Marekani, huku masomo yakisitishwa na waandamanaji wakikamatwa.

Maandamano hayo yaliyoanza wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Columbia yalihusisha kundi kubwa la waandamanaji walioanzisha kambi ya mshikamano na Gaza, na yalienea hadi kwenye vyuo vikuu vingine.

Wakati huo huo, Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema shambulizi la Israel kwenye ardhi ya Iran litaleta mabadiliko kamili ya hali ya mambo. Raisi ambaye yuko ziarani nchini Pakistan amenukuliwa Jumanne akisema shambulizi kama hilo linaweza kusababisha kusiwe na chochote kitakachosalia kuhusu "utawala wa Kizayuni".

(AFP, AP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW