Israel yakubali kuongeza muda wa kusitisha vita na Hamas
30 Novemba 2023Taarifa kutoka Qatar ambayo ndiyo mpatanishi mkuu zinasema nyongeza hiyo ya muda wa kusitisha mapigano imekubaliwa "chini ya masharti ya awali."
Taarifa hii ya kuongezwa muda huo inakuja wakati ambapo jeshi la Israel limesema mateka wengine sita zaidi wa Israel wamekabidhiwa Shirika la Msalaba Mwekundu na wako njiani kuelekea Israel. Hii inapelekea idadi jumla ya mateka wa Israeli walioachiwa hapo Alhamis kufikia watu 8.
Mapema Alhamis Hamas ambao wanaorodheshwa na Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine kama kundi la kigaidi, waliwakabidhi maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu mateka wengine wawili wa kike.
Herzog alimhimiza rais wa Emirati kutumia ushawishi wake
Haya yote yanafanyika baada ya Rais wa Israel Isaac Herzog kukutana na mwenzake wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan kandoni mwa mkutano mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa COP28, kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kwamba mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas wanaachiwa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Herzog imesema kwamba rais huyo wa Israel ametoa wito kwa rais Zayed Al Nahyan kutumia kikamilifu nguvu zake za kisiasa kuhakikisha kwamba mateka wanarudi nyumbani kwa haraka.
Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewaambia waandishi wa habari mjini Tel Aviv Alhamis kwamba, amekuwa muwazi kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba Israel inapaswa kuweka mikakati ya kuwalinda raia kabla kuanza tena operesheni yake kusini mwa Gaza.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amesema Israel, ni mojawapo ya jeshi lenye nguvu zaidi duniani ambalo lina uwezo wa kutuliza kitisho cha Hamas na wakati huo huo kupunguza hasara kwa watu wasio na hatia.
Blinken ameongeza kuwa Israel imekubaliana kuhusiana na suala hilo la kuwalinda raia.
Khan kuizuru Ramallah mbali na Israel
Hayo yakiarifiwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC imesema mwendesha mashtaka wake mkuu Karim Khan, anaizuru Israel kutokana na ombi la wahanga na familia za wahanga wa shambulizi la Hamas la Oktoba 7.
Mahakama ya ICC imeongeza kuwa Khan anatarajiwa pia kuizuru Ramallah katika Ukingo wa Magharibi kukutana na maafisa wakuu wa Palestina.
Katika ujumbe iliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, ICC imesema ziara hiyo si kwa ajili ya kufanya uchunguzi ila ni ziara inayotoa fursa ya kutoa pole kwa wahanga na kufanya mazungumzo nao.
Vyanzo: DW <https://www.dw.com/en/israel-hamas-war-truce-extended-new-hostage-list-sent/live-67590667 /> Reuters