1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yamuua afisa mwandamizi wa Fatah

21 Agosti 2024

Jeshi la Israel limeshambulia nchini Lebanon na kumuua afisa mwandamizi wa chama cha Fatah. Vuguvugu hilo la wanamgambo wa Kipalestina limeituhumu Israel kuwa inajaribu "kuchochea vita vya kikanda".

Rais wa Mamlaka ya Palestina na Kiongozi Mkuu wa Fatah Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Palestina na Kiongozi Mkuu wa Fatah Mahmoud AbbasPicha: Jordan TV/REUTERS

Mwanaharakati huyo mkuu wa kitengo cha kijeshi wa Fatah ni Khalil Maqdah ambaye ameuawa katika shambulio karibu na mji wa Sidon, kusini mwa Lebanon. Fatah, inayoongozwa na rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, ni vuguvugu la Kipalestina lenye makao yake katika  Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel.

Jeshi la Israel limesema lilikuwa likimlenga kaka yake Mounir Maqdah, ambaye anaongoza tawi la kijeshi la Fatah nchini Lebanon. Ndugu hao wawili wanashutumiwa na Israel kuendesha vitendo vya kusafirisha silaha na kuratibu mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi pamoja na kushirikiana na vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi vya nchini Iran.

Soma pia: Israel yathibitisha kumuua kamanda wa Fatah

Mjumbe wa kamati kuu ya FatahTawfiq Tirawy, ameliambia shirika la habari la AFP akiwa mjini Ramallah kwamba mauaji ya afisa wa Fatah ni uthibitisho wa ziada kuwa Israel inalenga kuchochea vita kamili katika eneo hilo.

Israel imeendelea kuishambulia GazaPicha: Ayman Al Hassi/REUTERS

Mauaji hayo ambayo ni ya kwanza dhidi ya afisa mwandamizi wa Fatah tangu kuanza kwa vita vya Gaza zaidi ya miezi 10 iliyopita, yanajiri huku mazungumzo ya kujaribu kuvimaliza vita vya Gaza yakiashiria kukwama.

Yote haya yanajiri wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiondoka mikono mitupu baada ya ziara yake huko Mashariki ya Kati iliyolenga kufikiwa kwa makubaliano ya usitishaji  vita kati ya Israel na kundi la Hamas huko Gaza.

Blinken ambaye alifanya ziara Israel, Misri na Qatar ameitolea wito Hamas kukubali haraka pendekezo la kusitisha mapigano linaloungwa mkono na Marekani. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani ameingia kwenye mzozo mpya na Israel kuhusu suala la uwepo wa jeshi la Israel katika ardhi ya Palestina mara baada ya vita hivyo kumalizika.

Vatican yatoa wito wa kuwepo amani duniani

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Ettore Ferrari/ANSA/picture alliance

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ameongoza hadhara yake ya kila wiki na ameutolea wito ulimwengu kuzingatia amani hasa wakati huu vita vikiripotiwa sehemu mbalimbali duniani:

" Tafadhali, tusiisahau Ukraine inayoteseka vibaya mno. Tusiisahau Myanmar, Sudan Kusini, Kivu Kaskazini, na nchi nyingi zilizopo kwenye vita. Tufanye maombi kwa ajili ya amani. Na tusizisahau Palestina na Israel."

Soma pia: Papa Francis ataka vita vya Gaza vikomeshwe

Hali inazidi kuwa mbaya huko Gaza, ambapo wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas ikisema kuwa idadi ya vifo sasa imefikia watu 40.223. Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema kifo ndio "chaguo" la mwisho kwa watu milioni 2.4 wa Gaza, kwa kuwa hakuna eneo lolote lililo salama wala njia ya kuepuka mashambulizi ya Israel.

(Vyanzo: DPAE, AP, Reuters, AFP)

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW