Israel yamuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah
1 Aprili 2026
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha kiusalama nchini Lebanon pamoja na kingine cha Hezbollah, vilivyozungumza na shirika la habari la AFP, kamanda huyo Youssef Hashem, aliyekuwa akihusika na masuala ya kijeshi ya kundi hilo nchini Iraq, aliuawa ndani ya hema wakati akifanya mkutano.
Jeshi la Israel limesema Hashem alikuwa kamanda wa Hezbollah katika mapambano ya kundi hilo kusini mwa Lebanon. Chanzo kingine kilicho karibu na Hezbollah kilisema Hashem ni "afisa wa ngazi ya juu kulengwa tangu kuanza kwa vita". Mwanachama mwingine wa kundi hilo Mohammad Baqir al-Naboulsi, pia ameuawa katika shambulizi lililofanyika eneo la Jnah mjini Beirut.
Israel pia imesema kuwa inataka kudhibiti tena eneo la kusini karibu na mpaka mwa Lebanon ili kuunda kile ambacho maafisa wamekitaja kama eneo la kiusalama ili kuwafurusha wapiganaji wa Hezbollah. Israel tayari ilikuwa inakalia eneo la kusini mwa Lebanon kwa karibu karne mbili hadi mwaka 2000. Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema Jumanne kwamba nyumba zote katika vijiji vilivyo kando na mpaka zitabomolewa. Lakini waziri mwenzake wa Lebanon Michel Menassa, amelaani mipango hiyo wakati Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney akisema ni "uvamizi usio halali."
Wakati huo huo, mvutano kati ya Marekani na washirika wake wa NATO umeongezeka baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa alikuwa akifikiria kuiondoa Marekani kutoka muungano huo wa kijeshi kutokana na wanachama wake wa Ulaya kukataa kutuma meli za kivita kwenda kufungua tena Mlango wa Hormuz.
Naye kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Mojtaba Khamenei ameapa hii leo kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono vikosi vinavyoipinga Israel katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati. Kauli hiyo kutoka kwa Khamenei, kama ilivyo kwa nyingine alizozitoa tangu achaguliwa kuwa kiongozi mkuu, imesomwa tu kupitia vyombo vya habari. Kiongozi huyo hajaonekana hadharani tangu vita vilipoanza Februari 28 huku maafisa wa Marekani na Israel wakiamini kwamba alijeruhiwa na anaendelea kujificha.
Hapo jana kituo cha habari cha RTVI, kilimnukuu Balozi wa Urusi aliyesema kuwa Khamenei yuko nchini Iran lakini anajizuia kujitokeza hadharani kutokana na "sababu zinazoeleweka".
Nalo jeshi la Walinzi wa Mapinduzi wa Iran IRGC limesisitiza Jumatano kwamba Mlango Bahari wa Hormuz, utaendelea kufungwa kwa ‘maadui' wa nchi hiyo, huku Rais wa Marekani Donald Trump akisema kwamba atazingatia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano endapo ungefunguliwa tena.