Israel yamuua kamanda mwingine wa kundi la Hezbollah
29 Septemba 2024Taarifa ya jeshi hilo limemtaja Kaouk kuwa kamanda wa kikosi cha kuzuia mashambulizi wa kundi la Hezbollah na alikuwa mjumbe wa Baraza la Uongozi la kundi hilo.
Israel imesema ameuawa kwenye shambulizi mahsusi lakini taarifa ya jeshi haikueleza wapi limetokea.
Tel Aviv inamtuhumu Kaouk kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel tangu alipojiunga na kundi hilo miaka 1980.
Jeshi la Israel limeapa kuendelea kuwaangamiza makamanda wa kundi la Hezbollah siku chache baada ya kufanikiwa kumuua kiongozi mkuu wa kundi hilo mjini Beirut
Hadi sasa Israel imeliangamiza karibu baraza lote la uongozi wa kundi la Hezbollah na kuharibu mengi ya maficho yake ya silaha.
Mauaji ya Nasrallah yafichua uwezo wa jeshi la Israel na udhaifu wa Hezbollah
Mauaji ya kiongozi mkuu na wa muda mrefu wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah yameakisi jinsi Israel ilivyomudu kuzima nguvu ya kundi hilo ndani ya muda mfupi.
Mauaji ya Nasrallah ya mwishoni mwa wiki hii yametokea wiki moja baada ya shambulizi kubwa la mtandao wa mawasiliano wa kundi la Hezbollah ambalo Israel ililaumiwa. Vifaa vya mawasiliano vya kundi hilo ikiwemo pager na simu za upepo viliripuka na kusababisha vifo na maelfu ya majeruhi.
Mauaji ya Nasrallah katika makao makuu ya kundi la Hezbollah mjini Beirut ilikuwa kilele cha mfululizo wa mashambulizi ya haraka ambayo yameondoa zaidi nusu ya baraza la uongozi la Hezbollah na kuangamiza kamandi yake ya juu ya kijeshi.
Siku chache kabla na saa kadhaa baada ya kuuawa kwa Nasrallah, shirika la habari la Reuters lilizungumza na duru kadhaa nchini Lebanon, Israel, Iran na Syria zikielezea hasara iliyosababishwa na Israel kwa kundi hilo lenye nguvu la wanamgambo wa Kishia, ikiwemo dhidi ya njia za ugavi na muundo wake wa uongozi. Wote walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina ili kuzungumzia masuala nyeti.
Chanzo kimoja chenye ufahamu kuhusu mawazo ya Israel kiliiambia Reuters, chini ya saa 24 kabla ya shambulio hilo, Israel imetumia miaka 20 kuelekeza nguvu za kijasusi kwa Hezbollah na inaweza kumlenga Nasrallah wakati inapotaka, ikiwa pamoja na katika makao makuu.
Mtu huyo aliitaja intelijensia hiyo kuwa ya "kiwango cha juu sana" bila hata hivyo kutoa ufafanuzi.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mawaziri wake wa karibu waliidhinisha shambulio hilo siku ya Jumatano, maafisa wawili wa Israel waliiambia Reuters. Shambulio hilo lilitokea wakati Netanyahu akiwa mjini New York kuzungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Nasrallah alitumia mbinu nyingi kuepuka mkono wa Israel tangu 2006
Nasrallah aliepuka kuonekana hadharani tangu vita vya awali vya 2006. Kwa muda mrefu alikuwa macho, mienendo yake ilikuwa imedhibitiwa na idadi ya watu alioonana nao ni ndogo sana, kulingana na chanzo kinachofahamu mipango ya usalama ya Nasrallah.
Mauaji hayo yameashiria kuwa kundi lake lilikuwa limeingiliwa na mashushushu wa Israel, chanzo hicho kilisema.
Kiongozi huyo wa Hezbollah amekuwa mwangalifu hata zaidi kuliko kawaida tangu milipuko ya pager ya Septemba 17, kutokana na wasiwasi kwamba Israel ingejaribu kumuua, chanzo cha usalama kinachofahamu mawazo ya kundi hilo kiliiambia Reuters wiki moja iliyopita, kikitaja kutokuwepo kwake kwenye mazishi ya makamanda na kurekodi kwake mapema hotuba iliyotangazwa siku chache kabla.
Rais wa Marekani Joe Biden, Jumamosi aliyataja mauaji ya Nasrallah kuwa "hatua ya haki" kwa waathirika wake wengi, na kusema Marekani inaunga mkono kikamilifu haki ya Israel kujilinda dhidi ya makundi yanayoungwa mkono na Iran.
Israel inasema ilifanya mashambulizi dhidi ya Nasrallah kwa kudondosha mabomu kwenye makao makuu ya chini ya ardhi yalioko chini ya jengo la makaazi kusini mwa Beirut.
"Hili ni pigo kubwa na kushindwa kwa intelijensia ya Hezbollah," anasema Magnus Ranstorp, mtaalamu wa siku kuhusu Hezbollah katika Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Sweden. "Walijua kwamba alikuwa katika mkutano. Alikuwa anakutana na makamanda wengine. Na wakamshambulia."