1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaongeza mashambulizi ya anga na ardhini Gaza

29 Desemba 2023

Israel imeshambulia maeneo ya kusini na katikati ya Ukanda wa Gaza leo Ijumaa, ambapo raia wa eneo hilo waliokimbia makazi yao wamelazimika kuyakimbia tena mashambulizi mapya ya anga na ardhini kutoka kwa Israel.

Ukanda wa Gaza | Wakaazi wakiwa kwenye malori wakiahama baada ya mashambulizi kuwafikia.
Wakaazi wa Gaza waliokimbia maeneo ya mapigano wakilazimika kuyahama makazi yao ya muda, baada ya vikosi vya Israel kushambulia.Picha: MOHAMMED ABED/AFP/Getty Images

Maelfu ya watu wa Gaza waliokimbia makaazi yao kutoka katika eneo la kusini mwa Ukanda wa Gaza walijibanza kwenye maturubai siku ya Ijumaa katika mji wa Deir al-Balah uliofurika watu, baada ya kukimbia mashambulio ya hivi punde kutoka katika wilaya za kati za Bureij, Maghazi na Nusseirat, zilizoshambuliwa na jeshi la Israel kwa vifaru na ndege za kivita.

Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina imesema watu 41 wameuawa katika mashambulizi ya Israel karibu na hospitali ya kusini mwa Gaza katika muda wa siku mbili zilizopita.

Ikijibu hayo jeshi la Israel limesema vikosi vyake vinaendeleza operesheni katika eneo la kusini la pwani katika mji wa Khan Yunis na kwamba limefaulu kuwaangamiza magaidi kadhaa katika muda wa saa 24 zilizopita.

Umoja wa Mataifa katika taarifa yake umesema maelfu ya Wapalestina wanaokimbia mapigano katikati ya mji wa Gaza wanaendelea kumiminika kwenye mji wa Rafah ambao pia umejaa watu.

Soma pia:Israel: Tumesikitishwa na shambulizi lenye madhara Gaza

Umoja wa Mataifaumesema mashambulizi ya anga na ya ardhini yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya kundi la Hamas yamesababisha asilimia 85 ya watu kati ya wakazi milioni 2.3 kuukimbia Ukanda wa Gaza.

Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza imeisema mpaka sasa Wapalestina wapatao 21,507 wameuawa na wengine 55,915 wamejeruhiwa.

Oparesheni za jeshi la Israel zachukua mwelekeo mpya

Israel inafunga mwaka kwa kufanya mashambulizi mapya katikati na kusini mwa Gaza, hali iliyofungua msafara mpya wa watu wanaokimbia vita. Watu hao tayari walikuwa wamekimbia vita kutoka kwenye maeneo mengine.

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

03:08

This browser does not support the video element.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant ameiita hiyo ni hatua muhimu ya dhamira ya nchi yake ya kulisambaratisha kundi la Hamas.

Wakati hayo yakiendelea Misri leo inatazamiwa kuwa mwenyeji wa wajumbe wa ngazi ya juu wa Hamas kwenye mazungumzo yenye lengo la kusitisha vita ambavyo vimesababisha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza.

Soma pia:Wizara ya afya Gaza yasema vifo kutokana na vita na israel vimefikia 21,320

Mkutano huo wa mjini Cairo unafanyika wakati mapigano yaliyochochewa na shambulio la Oktoba 7 yanapamba moto. Wanamgambo wa Hamas walivamia miji ya Israel na kuwaua watu 1,200 na kuwakamata mateka wengine 240. 

Vikosi vya Israeli vinarudisha mashambulizi kwa kuharibu sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW