Israel yaonya kuhusu mashambulizi makali dhidi ya Hezbollah
2 Novemba 2025
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema hii leo kwamba nchi yake itaongeza mashambulizi dhidi wa wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon. Taarifa ya kiongozi huyo inakuja siku moja baada ya wizara ya afya ya Lebanon kuripoti vifo vya watu wanne katika shambulio la anga la Israel.
Tangu kupatikana kwa makubaliano ya usitishaji vita mwaka uliopita, serikali yaLebanon imekuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa Israel na Marekani la kutakiwa kulipokonya silaha kundi la Hezbollah, mpango unaopingwa na kundi hilo na washirika wake.
Katikati mwa mwezi Oktoba Rais wa Joseph Aoun wa Lebanon alituma ombi la kutaka kufanya mazungumzo na Israel baada ya Rais wa MarekaniDonald Trump kusaidia kuratibu usitishaji mapigano huko Gaza. Lakini baadaye Aoun aliishutumu Israel kwa kuitikia ombi lake hilo kwa kuongeza mashambulizi yake ya anga nchini mwake.