Israel yaonya silaha za Syria kuangukia Hizbullah
9 Februari 2012Kwa mujibu wa maelezo ya wanaharakati wa kambi ya upinzani mjini Beirut, idadi kubwa ya vifo hivyo vimetokea katika maeneo ya Khalidiyeh na Baba Amr. Akithibitisha tukio hilo, Rami Abdel Rahman wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Syria, amesema mashambulizi hayo yaliyoanza siku ya Jumamosi yamekwishaua zaidi ya watu 400 mpaka sasa.
Mwanaharakati mwingine, Omar Shaker, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa kwa njia ya simu kuwa wakazi wa jirani na Homs wanajificha sehemu ya chini ya majengo yenye ghorofa kutokana na kutokuwepo na mahandaki ya kujihami na mashambulizi hayo.
Kufuatia mauaji hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon, amesema Umoja wa Mataifa umeshasikia ahadi nyingi ambazo hazijatekelezeka hata katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
"Ninaamini hali mbaya inayoshuhudiwa Syria italiathiri eneo lote jirani. Na mpaka vitokee vifo vingapi ndio hatua ya kukomesha ukatili huu unaosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe ichukuliwe?" Amehoji Ban Ki-moon.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema serikali ya nchi yake inachunguza kwa makini mwenendo wa jeshi la Syria kwa lengo la kuhakikisha silaha zake hazisafirishwi nchini Lebanon na kukabidhiwa kwa wapiganaji wa Hizbullah.
Barak ametoa onyo hilo leo kupitia radio ya jeshi la Israel, akiongeza kuwa Israel inaamini kuwa serikali ya Bashar al-Assad itaangushwa wakati wowote kuanzia sasa.
Taifa la Israel linafuatilia kwa karibu mauaji yanayotokea Syria ambapo watu zaidi ya 6,000 wameuwawa na askari wanaomtii Assad, miezi 11 tangu maandamano ya kuupinga utawala wake yaanze.
Serikali hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, inahofia usalama wake kufuatia ghasia za Syria, na uwezekano wa taifa hilo la Kiyahudi kuvamiwa na maelfu ya wakimbizi kuingia nchini humo kuokoa maisha yao.
Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alililaumu Jeshi la Syria kwa kuendelea kutumia ukatili na kuua raia 69 hapo jana na akasema Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inapendekeza kutumwa kwa ujumbe wa pamoja ili kushuhudia mauaji hayo, mjini Homs.
Nao mawaziri wa nchi za Kiarabu wanatarajia kukutana hapo Jumapili mjini Cairo, Misri kujadili uwezekano wa kulitambua Baraza la Taifa la Syria na namna ya kumaliza ghasia.
Mwandishi: Pendo Paul\dpa\AFP
Mhariri: Mohammed Khelef